Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amewaagiza madiwani wa Halmashauri zote nchini
humo kudhibiti wizi wa dawa katika hospitali na vituo vingine vya afya nchini. Aidha,
Rais Kikwete amewaagiza madiwani kuanza kuweka kwenye bajeti za halmashauri zao fedha
za kujengea nyumba za walimu wa shule mbalimbali nchini kama njia ya haraka ya kumaliza
tatizo la uhaba wa nyumba za walimu.
Pia Rais Kikwete amesema kuwa mbali
na walimu, ni wajibu wa madiwani na Halmashauri nchini kuweka katika bajeti zao fedha
za kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka mbali na shule wanazosoma ama
wanaoishi katika mazingira hatarishi. Rais Kikwete ametoa maelekezo hayo, Ijumaa,
Julai 26, 2013, wakati alipozungumza na wananchi wa Biharamulo mjini kabla ya kuweka
jiwe la msingi la Barabara ya Kagoma-Lusahunga.
Akizungumza kwenye sherehe
hizo zilizofanyika nje ya Mji wa Biharamulo kwenye njia panda ya kwenda Lusahunga,
Rais Kikwete amewaambia madiwani kuwabana watendaji katika halmashauri mbalimbali
na kusimamia usambazaji waharaka na usiokuwa na wizi wa dawa. “Taarifa hizi za wizi
wa dawa zinaudhi sana. Serikali inahakikisha kuwa inatoa dawa za kutosha lakini bado
dawa hizo haziwafikii wananchi.
Wakati mwingine mtu anakwenda hospitali, anaandikiwa
dawa na kuelekezwa aende kwenye duka la dawa kumbe duka lenyewe ni mali ya aliyeandika
hiyo karatasi ya maelekezo ya dawa. Kuna udanganyifu mwingi na madiwani lazima watusaidie,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kuhusu uhaba huu wa nyumba za walimu ni
vyema kuwa halmashauri zetu nchini kuanza kujihusisha na ujenzi huo kwa kuweka katika
bajeti zao fedha za kujenga nyumba za walimu. Hawa ni walimu wako chini ya Halmashauri
sasa inakuwaje halmashauri zisijihusishe na ustawi wao?”
Mapema, Waziri wa
Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli amewaasa viongozi wa Halmashauri nchini kuhakikisha
kuwa wanatumia fedha nyingi ambazo wanapewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara
katika maeneo yao lakini wanashindwa kutumia fedha hizo.
“Tunatoa fedha nyingi
kutoka kwenye Road Fund lakini viongozi wa Halmashauri mbalimbali wanashindwa kuzitumia
na badala yake unafika mwisho wa mwaka wa fedha wakati fedha hizo bado ziko mikononi
mwao na wananchi wanaendelea kulalamikia barabara mbovu. Hizi siyo fedha zao, ni fedha
za wananchi kwa ajili ya ustawi wao kwa kuwajengea barabara.”