2013-07-28 07:45:34

Viongozi wanachangamotishwa kuwajibika kijamii, wakiwa na sera na mikakati inayowashirikisha watu!


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 27 Julai 2013 alipata pia fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanasiasa na Wasomi kutoka Brazil na kuwataka kutekeleza wajibu wao kwa Jamii katika jicho la ukweli, huku wakionesha utulivu, amani na hekima. Haya ni mambo ambayo yanapata chimbuko lake katika utamaduni, uwajibikaji wenye kujenga na kuimarisha mshikamano kati ya watu ili kujenga kesho iliyo bora zaidi pamoja na mchakato wa kuimarisha majadiliano ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu anawahimiza wasomi hawa kuenzi utamaduni unaotoa utambulisho wa wananchi wa Brazil, kwa kuchangamana, daima wakitafuta mafao ya wengi, kwani hapa ni mahali ambapo: imani na fikira za mwanadamu zinakutana na kukumbatiana; hapa ni mahali tunu mbali mbali za maisha ya mwanadamu na utamaduni wake; sanaa na sayansi; kazi na fasihi vinaunganishwa katika Ukristo na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha bila kukata tamaa, hali ambayo inajikita katika mioyo ya watu wengi kwa sasa.

Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza viongozi hawa kuwajibika kijamii, wakiwa na sera na mikakati ya kiuchumi, kisiasa na kijamii inayowashirikisha watu katika kutafuta hatima ya maisha yao kwa siku za usoni, sanjari na kupambana na baa la umaskini bila kutumbukia katika utawala wa mabavu. Viongozi wanapaswa kuwa na dira na mikakati makini inayotekelezeka bila kukata tamaa pale malengo haya yanapoyeyuka na kubaki kuwa ni ndoto tu!

Hapa anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya kujenga na kudumisha fadhila ya matumaini ili kujenga mazingira yatakayomwezesha kiongozi kufikia malengo yake hata kama itachukua kitambo kidogo. Viongozi wawe na ujasiri wa kuchagua kwa haki vipaumbele wanavyotaka kutekeleza kwa kuwajibika na kwa ajili ya mafao ya wengi. Viongozi katika uwajibikaji wao ambao pengine unakumbana na mapungufu, lakini jambo la msingi ni kufahamu ukweli wote unaopaswa kufanyiwa upembuzi yakinifu, ili kufanya maamuzi ya busara yenye athari zake kwa sasa na kwa siku za usoni.

Kiongozi anayetenda kwa busara anapaswa kujipima mbele ya haki za wengine na mbele ya Mwenyezi Mungu. Huu ni wajibu wa kimaadili ambao unaonekana kuwa ni changamoto kubwa mbele ya ulimwengu mamboleo. Haitoshi kufanya maamuzi kwa kuikita katika misingi ya kisayansi na kiufundi bila kujihusisha na kanuni maadili inayomwajibisha mtu kijamii ili kujenga mshikamano wa dhati.

Baba Mtakatifu anawaalika wasomi na wanasiasa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano yanayojenga kama njia ya kujiepusha na ubinafsi au kwa kuelemewa na matumizi ya nguvu. Majadiliano ni njia muafaka kati ya kizazi kipya na kati ya Jamii ya watu, kwani huu ni uwezo wa kutoa na kupokea, daima wakiwa wazi na makini katika ukweli.

Jamii inaweza kukua na kupanuka ikiwa kama inajenga na kudumisha majadiliano ya kweli yanayojikita katika utajiri unaofumbatwa katika tamaduni, mapokeo, sanaa, teknolojia, uchumi, familia na njia za mawasiliano. Hakuna matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi anasema Baba Mtakatifu bila ya kuzingatia kanuni maadili na demokrasia inayopania ustawi na maendeleo ya wengi. Hapa kuna haja ya kupokea mchango unaotolewa na Mapokeo ya dini mbali mbali duniani yanayoendelea kuchangia ustawi na demokrasia.

Kuna haja ya kudumisha amani na utulivu, kwa kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kuthaminiana na kuheshimiana miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; viongozi wawe na ujasiri wa kuheshimu na kuthamini tunu msingi za maisha ya kiroho yanayojionesha katika uhalisia wa maisha, hata kama kiongozi huyo haoni kuwa huo ni msimamo wake wa kidini.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, Wanasiasa na Wasomi kwa kusema kwamba, ili mtu, familia na jamii iweze kukua na kukomaa katika tunu msingi za maisha, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikishana yale mazuri na mema yanayopatikana katika maisha ya watu.







All the contents on this site are copyrighted ©.