2013-07-27 08:29:28

Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu!


Njia ya Msalaba ni kati ya matukio makuu yanayopamba Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, tangu mwaka 1984, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alipowakabidhi vijana Msalaba, ambao umetembelea Mabara yote. Hakuna anayeweza kugusa Msalaba wa Kristo bila kuacha sehemu ya maisha yake na kupokea neema kutoka kwa Kristo.

Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Njia ya Msalaba kwenye ufuko wa Copacabana, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Baba Mtakatifu anawauliza vijana wa Brazil baada ya kutembeza Msalaba huu kwa takribani miaka miwili, ni mambo yepi ambayo wameacha chini ya Msalaba? Baba Mtakatifu anaendelea kuwauliza vijana wenyewe ni mambo yepi ambayo Kristo amewaachia wakati walipokuwa wanautembeza Msalaba huo? Mwishoni, Baba Mtakatifu anawauliza vijana maana ya Msalaba katika maisha!

Baba Mtakatifu anasema, Msalaba unatisha, kama ilivyojionesha hata kwa Mitume wa Yesu, waliotaka kukimbia madhulumu ya Nerone; Petro kwa mshangao mkubwa akakutana na Yesu njiani akielekea mjini Roma ili aweze kusulubishwa mara ya pili; hapo ndipo Mtume Petro alipoishiwa nguvu, akapiga moyo konde na kufuata nyayo za Kristo, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba kwa kutambua kwamba, Yesu alikuwa amempenda upeo!

Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Msalaba, Yesu anajiunga na wale wote wanaodhulumiwa na kuteswa; watu ambao hawana tena nguvu ya kupiga kelele; hasa watu wasiokuwa na hatia wala ulinzi madhubuti; familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha; wale wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao katika maisha; wanaowalilia watoto wao waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anaungana na mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa wakati ambapo kuna sehemu nyingine za dunia wanakula na kusaza! Anajiunga na wale wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani, mawazo na rangi ya ngozi. Yesu anaendelea kujiunga na umati mkubwa wa vijana uliopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na wanasiasa wanaowaongoza kuelemewa mno na ubainfsi, rushwa na ufisadi.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwaambia vijana kwamba, Yesu anaendelea kuungana kwa njia ya Fumbo la Msalaba na waamini ambao wamepoteza imani yao kwa Mungu na Kanisa kutokana na kashfa na utepetevu wa imani ulioneshwa na watumishi wa Injili. Yesu anayapokea yote haya kwa mikono miwili na kujitwika mabegani mwake pamoja na Misalaba ya wafuasi wake, tayari kuwaambia, jipeni moyo kwani yuko pamoja nao na kwamba, ameshinda dhambi na mauti na yuko kati yao ili kuweza kuwakirimia matumaini na maisha tele!

Baba Mtakatifu Francisko anawauliza vijana ni mambo yepi ambayo Fumbo la Msalaba limewaachia baada ya kuuona na kuugusa Msalaba ulipokuwa unatembezwa mitaani na kwenye viunga vyao vya maisha? Jibu makini linajikita katika upendo wa Mungu kwa binadamu wote.

Ni upendo ambao unapenya katika mapungufu na dhambi za mwanadamu kiasi cha kumkirimia msamaha; upendo unaopenya katika taabu na mahangaiko ya binadamu kiasi cha kumjalia nguvu ya kuweza kuyabeba na kuyavumilia; upendo umegusa hata mauti, na kuyashinda na hatimaye kumkirimia mwanadamu maisha ya uzima wa milele.

Yesu anawajalia wafuasi wake matumaini na maisha tele! Amegeuza ile kashfa ya Msalaba ulioonekana kuwa ni chombo cha chuki na uhasama, anguko na kifo, kuwa ni alama ya ushindi na maisha. Hakuna Msalaba mdogo wala mkubwa katika maisha, bali ni uwepo endelevu wa Kristo anayetaka kushiriki na kuwamegea wafuasi wake maisha na uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anasema, Msalaba ni mwaliko wa Kristo kwa wafuasi wake ili waweze kuguswa na upendo wa dhati unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Ni changamoto ya kuendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo; hasa zaidi kwa wale wanaoteseka; watu wanaohitaji msaada; ni jukumu la kila mwamini kujitoa katika ubinafsi wake ili kuwaendelea na kuwanyooshea mikono tayari kuwasaidia wengine.

Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, hata wao wanaweza kuwa kama Pilato anayeelemewa na woga kiasi cha kushindwa kuokoa maisha ya Yesu dhidi ya kifo, anajiondoa kwenye hatia hii kwa kunawa mikono yake! Fumbo la Msalaba ni mwaliko kwa kila mwamini kuwa kama Simoni wa Kirene, aliyemsaidia Yesu kubeba Msalaba, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na kwa wanawake wengine watakatifu, waliopiga moyo konde, wakaifuata ile njia ya uchungu wakiwa wamesheheni upendo na huruma hadi chini ya Msalaba.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha tafakari yake wakati wa Njia ya Msalaba kwenye ufuko wa Copacabana kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa kumuuliza kila kijana, anajisikia kuwa ni nani katika Njia hii ya Msalaba: Pilato, Simoni wa Kirene au Bikira Maria?







All the contents on this site are copyrighted ©.