2013-07-26 09:40:39

Wamemwona, wamemsikia na kuguswa na uwepo wake!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 25 Julai 2013 aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa Waseminari wakuu pamoja na Walezi wao; ibada ambayo imehudhuriwa na zaidi ya Majandokasisi 300. Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yakobo Mtume, Baba Mtakatifu amewakumbusha Waseminari kwamba, wito wao ambao ni kito cha thamani kubwa, umehifadhiwa katika chombo cha udongo.

Hii ni kutokana na udhaifu na mapungufu ya binadamu, changamoto na mwaliko kwa Makleri kujipatanaisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio; Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu akiwa kwenye Majengo ya Manispaa ya Jiji la Rio de Janeiro, alibariki bendera kwa ajili ya michezo ya Olympic. Tukio hili limehudhuriwa na baadhi ya wanamichezo maarufu kutoka Brazil, lakini hakuwepo Pele, mchawi wa kabumbu enzi zake, kama wengi ambavyo walidhani ingeweza kutokea.

Baba Mtakatifu Francisko alibahatika kutembelea Familia moja katika kitongoji cha Varginha na kusalimiana nao! Hii ni familia inayoshiriki katika utume wa Biblia, hata Baba Mtakatifu mwenyewe anasema ameshangazwa na jinsi ambavyo katika hali yao wanavyoifahamu na kuimwilisha Biblia katika maisha yao ya kawaida pasi na makuu wala makeke ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anakaribia kuondoka, anasema Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican aligundua kwamba, alikuwa bado hajamuaga Paroko, akalazimika kusimamisha gari na kwenda kuomba masamaha kwa Paroko na baadaye akamuaga na msafara ukaondoka. Hiki ni kitendo cha unyenyekevu, lakini pia ni heshima kwa wenyeji wa eneo hili. Familia iliyotembelewa na Baba Mtakatifu ina jumla ya watu 20.

Baba Mtakatifu aliweza kuzungumza na kubadilishana mawazo na Familia ya Mungu kutoka katika kitongoji hiki, tukio ambalo limehudhuriwa pia na viongozi wa Kanisa la Kiinjili, ambao wamemwomba Baba Mtakatifu kubariki maji watakayotumia katika Ibada zao!

Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Argentina, akawahimiza kutoka mafichoni walikojificha ili kuwa kweli ni Wamissionari wa Yesu, hata kama mwaliko huu una madai yake, lakini wanapaswa kwenda kumtangaza Kristo hadi miisho ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.