2013-07-26 07:22:04

Utajiri wa mtu unajikita katika moyo wake na wala si vitu au mali aliyo nayo!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 25 Julai 2013 ametembelea Jumuiya ya Varghinha, baada ya sala na tafakari kwa kitambo kidogo, alibariki Altare mpya ya Kanisa la Mtakatifu Girolamo Emiliani na baadaye akatoa zawadi ya Kalisi mpya kwa Parokia hii.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake anasema, katika hija yake kitume nchini Brazil angependa kutembelea kila sehemu na kusalimiana pamoja na kushiriki ukarimu wa wananchi wa Brazil, kumbe Jumuiya ya Varginha ni kielelezo cha utashi huo unaobubujika kutoka katika undani wake na kwamba, kuna haja ya kujenga na kuimarisha ukarimu katika maisha kama kielelezo cha mshikamano wa upendo unaowawezesha waamini kutajirishana hata katika kile kidogo walichonacho! Utajiri wa mtu unafumbatwa si katika vitu na mali aliyo nayo, bali yale yaliyomo moyoni mwake!

Brazil anasema Baba Mtakatifu ni nchi ambayo inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini bado inaonesha moyo wa ukarimu na mshikamano ambao wakati mwingine hakuna anayeuona wala kuupigia debe! Kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake, anachangamotishwa kuhakikisha kwamba, anasimama kidete kukomesha mambo yote yanayosababisha ukosefu wa haki jamii, unaojengwa kutokana na ubinafsi pamoja na umimi unaoendelea kuharibu dunia. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano wa upendo kwa kumwona kila mtu kuwa ni jirani yako mwema!

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwatia shime wananchi wa Brazil kujitosa kimasomaso katika mapambano dhidi ya njaa na umaskini, kwa kuwashirikisha wananchi wote wa Brazil katika mchakato wa ustawi na maendeleo endelevu. Kwa kushirikishana na kumegeana hata kile kidogo walichonacho, Jamii itajikuta ikitajirishana.

Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuchangia kwa hali na mali, kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi wa Brazil: kiroho na kimwili, kwa ajili ya mafao ya wengi, kwa kutambua, kulinda na kuthamini uhai zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; tunu msingi za maisha ya kifamilia; elimu makini, sera bora za huduma ya afya bila kusahau mahitaji ya wananchi wa Brazil katika maisha ya kiroho na kwamba, amani na utulivu vinapata chimbuko lake katika moyo wenye toba na wongofu wa ndani.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia vijana kwamba, wanayo dhamana ya kupambana na maovu katika Jamii, lakini jambo la kusikitisha ni kuona pale ambapo vijana wanakata na kujikatia tamaa kuhusiana na mambo ya rushwa, ufisadi na ubinafsi, badala ya kutafuta mafao na ustawi wa wengi. Baba Mtakatifu anawaambia vijana kutokata tamaa wala kuzima mshumaa wa matumaini yao, kwani mambo yanaweza kubadilika.

Vijana wanapaswa kuwa wa kwanza katika kutafuta mafao ya wengi; kwamwe wasifurahie kuogelea katika mabaya, bali wasimame kidete kupinga maovu, wakitambua kwamba, katika mapambana haya, Kanisa pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro wako nao bega kwa bega!

Wakati huo huo, Jumuiya ya Varginha iliyoanzishwa kunako mwaka 1940 kwenye eneo la taka ni kielelezo cha ushuhuda wa maisha ya Baba Mtakatifu Francisko anayewapenda na kuwajali maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; watu ambao wamesahauliwa na Jamii. Maisha ya watu hawa bado ni tete, kwani hawajafaulu kuishi kwa heshima na utu kama binadamu.

Uwepo wa Baba Mtakatifu wanasema wenyeji hawa umewaletea nafuu ya maisha kwani kuna mabadiliko makubwa. Ni matumaini yao kwamba, mara baada ya ugeni wa Baba Mtakatifu hali ya maisha itaendelea mbele kama ilivyo kwa sasa! Wanashukuru Baba Mtakatifu kwani wao leo hii wamekuwa ni sehemu ya habari za Kimataifa. Ni Jumuiya inayopewa kipaumbele cha kwanza pale yanapotokea mafuriko na hivyo kusababisha maafa makubwa au kunapokuwepo na mapambano ya silaha.

Wenyeji hawa wamemwambia Baba Mtakatifu kwamba, Mwenyezi Mungu daima amewangalia hata katika unyonge wao. Kunako mwaka 1971, Kikanisa cha kwanza kilitabarukiwa katika eneo hili na kuwekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Girolamo Emiliani aliyetangazwa na Papa Pio wa Kumi na moja kuwa Msimamizi wa Watoto Yatima na Vijana wanaoishi katika Mazingira hatarishi.

Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza pia ushuhuda wa Familia ya Bwana na Bibi Rangler dos Santos Irineu na Joana Alves de Souza Carvalho wanaotekeleza utume wao Parokiani; hii ni familia ndogo, maskini na iliyosahauliwa machoni pa binadamu, lakini imepata kuonja ukuu wa Mungu, wao wataendelea kuwa waaminifu kwa Mungu, wakiwa wameungana kama Bwana na Bibi kwani hata maskini wanaweza kupata utambulisho wao kwa njia ya Papa Francisko.







All the contents on this site are copyrighted ©.