2013-07-26 11:01:46

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa


Kama kawaida tunakutana tena katika kipindi chetu tafakari masomo Dominika. Tayari tuko Dominika ya 17 ya Mwaka C. Katika Dominika hii Bwana anatufundisha namna ya kusali. Anafundisha sala ya Baba yetu kama kielelezo cha sala nyingine zote. RealAudioMP3

Akishafundisha sala, ataenda hatua ya pili ya sala yaani kudumu katika kuomba ili kuweza kujenga urafiki na Mungu, urafiki wa kudumu. Kwa hakika anakazia umuhimu wa kuomba na matokeo yake lazima yawe ni mazuri, yaani Mungu hawezi kutoa kitu kibaya kwa yule anayeomba bali hutoa anachostahili. Ndiyo kusema mkazo katika maisha ya sala waruhusu mto wa zawadi za Kimungu kwetu kwa yule anayesali na kwa yule anayeombewa.

Mpendwa mwana wa Mungu, Mitume wanamwomba Bwana awafundishe kusali. Tunajiuliza ni kwa nini ombi hilo? Wanafikia ombi hilo kwa sababu kulikuwa na makundi mbalimbali yaliyokuwa yana namna yao ya kusali. Mojawapo ya makundi haya ni kundi la Mafarisayo na kundi la Yohane Mbatizaji. Si hilo tu bali hasa walivutwa na namna ya Bwana mwenyewe alivyokuwa akiwasiliana na Baba yake akitumia neno “Abba” maana yake Baba kwa Kiaramaiki.

Hawaishii katika kuvutwa na neno Abba bali ni kitu gani Bwana anataka kujenga katika mantiki ya kutumia neno hilo. Neno hilo linalenga kukuza uhusiano wa Baba na mtoto wake. Linakuza uhusiano wa ndani kabisa ambao katika hali ya kawaida hatuwezi kuufikia.

Mpendwa, baada ya ombi la Mitume wakimwomba Bwana awafundishe namna ya kusali, jibu linalotoka ni jibu la kushangaza yaani badala ya kuja na sala ndefu anakuja na sala fupi na rahisi. Mara moja tunajifunza kuwa jambo la maana si urefu wa sala bali ROHO ya sala, yaani mzizi na kiini cha sala yenyewe. Roho ya sala ya Baba yetu ni neno Abba.

Pamoja na kwamba Mungu ni mkuu lakini wadogo wanamfikia bila pingamizi. Wanakuwa karibu naye na wanajisikia watoto wake wakisema Abba! Kumbe mpendwa msikilizaji jambo la maana si kuunda sala katika muundo wa kimahesabu bali kutafuta daima ROHO ya Kiinjili yaani roho ya kujisikia mtoto wa Mungu, na kwa namna hiyo kuita jina la Bwana kwa unyenyekevu kama Bwana alivyofanya daima.

Mpendwa, sala yako yapaswa kuwa sala inayoomba neema ya kujifunza upya daima, kusema kwa furaha na tumaini lile neno muhimu yaani Abba. Sala yako iwe kama sala ya Bwana ambayo imfikiapo Baba wa Mbinguni hushusha neema kwa ajili ya wengine, kama Abrahamu alivyofanya kama tusomavyo katika somo la I. Sala yako lazima iwe katika mfumo ambao umejengwa tayari katika Injili ya leo. Angalia, kuna watu watatu: yule anayeamshwa usiku, yule anayemwamsha mwenzake na yule aliyefika usiku yaani mwenye mahitaji, mwenye taabu.

Basi hapa tunaona yule wa pili anaomba kwa ajili ya yule wa tatu na yule wa kwanza anasikiliza na kuitikia. Sala ni kwa ajili ya wanaoteseka na kughubikwa na taabu mbalimbali. Huyu mtu wa tatu anayefika usiku ni kiwakilishi cha watu wote wenye shida mbalimbali katika maisha yao.

Sala yapaswa kujitokeza katika huduma ndiyo maana huyu anayesali anahangaika ili mwenye taabu apate hifadhi. Kumbe, kama mmoja anasema mimi nawaombea wagonjwa pasipo kwenda kuwaona hospitali au majumbani bado sala yake ina walakini. Yote haya yanafanyika katika Kristo Bwana mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote na kwa njia yake vyote vilifanyika na vinaendelea kufanyika.

Nikutakie maisha mema ya sala na tafakari daima inayojitokeza katika kuwahudumia wengine. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.