2013-07-26 09:13:38

Kila kijana anaweza kuwa ni shahidi wa upendo na ujasiri wa Injili ya Kristo ili kupeleka mwanga katika ulimwengu mamboleo!


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika vijana kujenga utamaduni wa kumsikiliza Kristo kwa umakini mkubwa, ili waweze kumpokea na kumkaribisha katika hija ya maisha ya ujana wao. Yesu ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu anawaletea mabadiliko na anawaangazia katika mapito yao kwa siku za usoni.

Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kukuza ndani mwao fadhila ya matumaini ili waweze kutembea kwa furaha! Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya wakati wa sehemu ya pili ya tafakari yake kwa ajili ya kuwakaribisha vijana kwenye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.

Baba Mtakatifu anawataka vijana katika safari ya maisha yao ya ujana kutoa kipaumbele cha pekee kwa imani, matumaini na mapendo, ili kujenga maisha yao katika mwamba thabiti na hivyo kutembea kwa furaha sanjari na kukutana na marafiki wengine wanaofanya hija pamoja nao! Fadhila hizi zinapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo, kiasi kwamba, vijana wanaweza kuuangalia ukweli wa maisha kwa ujasiri mkubwa, kwani Yesu Kristo ni rafiki na mwenza anayeaminika.

Huu ni mwaliko kwa vijana kumpokea na kumruhusu Kristo kuwa kweli ni dira na mwongozo wa maisha yao. Kuna vijana wengi wanaotaka kujenga maisha na kuwa na furaha inayojikita katika mali na madaraka, lakini haya ni mambo ya mpito, ikiwa kama Kristo atakuwa ni nguzo ya maisha ya kijana, kamwe kijana huyu hataweza kudanganyika.

Imani inamwezesha mwamini kuona mabadiliko na kuwa na usalama, nguvu na matumaini. Bila ya uwepo wa Mungu, maisha ya mwanadamu ni ubatili mtupu! Baba Mtakatifu anawaambia vijana katika sakafu ya mioyo yao kuna matunda ya Roho Mtakatifu ambayo ni: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Mwamini akimruhusu Yesu kutenda kazi ndani mwake atafanikiwa kuwa ni shahidi amini wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Siku ya Vijana Duniani inakuwa ni zawadi kubwa kwa vijana ili kuweza kumkaribia zaidi Kristo, ili kuwa kweli ni wanafunzi na wamissionari wake, huku wakiendelea kutoa nafasi kwa Kristo aweze kuwaletea mabadiliko ya kweli katika maisha!

Kwa msisitizo mkubwa, Baba Mtakatifu anawaalika vijana kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo, kwa njia ya kumsikiliza kwa makini, kumpokea katika Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, katika Sakramenti ya Upatanisho, ili aweze kuwaganga majeraha ya dhambi kwa njia ya huruma yake. Kamwe vijana wasiogope kumwomba Mungu msamaha wa mapungufu ya maisha yao, kwani Mwenyezi Mungu daima yuko tayari kuwasamehe dhambi zao, kwani anawapenda na mwingi wa huruma.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kumpokea Kristo katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, inayoonesha uwamo wake endelevu katika Maumbo ya Mkate na Divai; Sadaka ya Mapendo na chemchemi ya urafiki wa kina utakaoendelea kuyatajirisha maisha ya vijana kwa njia ya ushuhuda wa imani; watafundishwa lugha ya upendo, wema na huduma. Kila kijana anaweza kuwa ni shahidi wa upendo na ujasiri wa Injili ya Kristo ili kupeleka mwanga katika ulimwengu mamboleo.

Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, inapendeza kukaa hapa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo anayewakirimia: imani, matumaini na mapendo. Anawaalika vijana kuwa kweli ni Wamissionaro wa Kristo kwa kukubali mwaliko na wito wake, ili waweze kumpenda na kumfanya Kristo apendeke zaidi. Yesu anawasubiri na kwamba, ana matumaini makubwa kwa vijana!







All the contents on this site are copyrighted ©.