2013-07-25 09:41:24

Utengano ndani ya Kanisa unaweza kupatiwa tiba kwa njia ya huruma ya Mungu


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa vatican ni fursa ya kuangalia mchango wa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. RealAudioMP3

Mababa 200 kutoka Kanisa la Mashariki walihudhuria Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakaweka msingi wa ushirikiano na majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa.

Ni Mababa ambao wamechangia kwa namna ya pekee, katika Maadhimisho haya wakitambua dhamana yao katika kujenga na kudumisha uhusiano ndani ya urika wao kama Maaskofu, kielelezo cha umoja katika Makanisa mahalia pamoja na Kanisa la Kiulimwengu wanapoungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye ni kielelezo cha kifungo cha amani, upendo na umoja. Maaskofu wote wanawajibika kukuza na kulinda umoja wa imani na nidhamu pamoja na mshikamano wa upendo kwa maskini na wote wanaodhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia.

Maaskofu wanapaswa kushikamana kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Utofauti wa Makanisa mahalia yaliyo na umoja kati yao unadhihirisha zaidi Ukatoliki wa Kanisa lisilogawanyika.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kuhamasisha umoja na udugu kwa Makanisa ya Mashariki yaliyojitenga ili kuweza kuungana kiimani kwa kuzingatia kanuni na sheria za Kanisa zilizopo. Kuna uwezekano pia kwa Waamini wa Kanisa la Mashariki kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Useja na Ndoa kwa Makleri wa Kanisa la Mashariki ni sehemu ya wito wao unaopaswa kuheshimiwa katika mchakato wa kujenga na kuimarisha Kanisa la Kristo. Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kunako mwaka 1990 aliridhia Sheria za Kanisa la Mashariki, kiini cha sheria hizi ni umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni mchango wa Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kama ulivyoandaliwa na Ubalozi wa Romania mjini Vatican. Juhudi za majadiliano ya kiekumene zinapania pia kuchota utajiri mkubwa unaopatikana katika Liturujia ya Makanisa ya Mashariki; maisha ya kiroho, nidhamu na taalimungu.

Katika utofauti huu utume na ukatoliki wa Kanisa unajidhihirisha wazi; kila upande ukiwa na haki sawa pamoja na dhamana ya kutekeleza. Huu ulikuwa ni mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mambo yote haya anasema Kardinali Sandri yanaratibiwa na mwongozo uliotolewa na Bara la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki mwa Mwaka 1996 unaozingatia pia Sheria za Kanisa la Mashariki kwa kuhimiza uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Neno la Mungu halibadiliki, lakini mwanadamu anabadilika kutokana na historia na nyakati, changamoto ya kusoma alama za nyakati.

Kwa muhtasari Kardinali Sandri anasema haya ndiyo mawazo makuu yaliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuonesha kwanza kabisa: maisha ya kiroho yanayofumbatwa katika sala na Mapokeo ya Kanisa la Mashariki, daima iwe n changamoto kwa waamini kutafuta Umoja wa Kanisa. Utengano ndani ya Kanisa unaweza kupatiwa tiba kwa njia dawa ya huruma ya Mungu, kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu.

Dhambi na upotofu virekebishwe; mdhambi aonjeshwe upendo na huruma ya Mungu. Kwa pamoja, Makanisa haya yajikite katika mchakato wa Uinjilishaji kama alivyobainisha Papa Paulo wa Sita; changamoto inayoendelezwa na Mama Kanisa kwa sasa katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Kardinali Sandri anasema kwamba, umoja wa Kanisa ndiyo changamoto endelevu inayopaswa kufanyiwa kazi na Makanisa kwa njia ya ushuhuda wa imani katika matendo. Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki ni amana kubwa kwa Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Wakristo wanapaswa kuonesha ushindi wa Msalaba wa Kristo, chemchemi ya huruma, upendo na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Umoja na Mshikamano wa Wakristo uwe ni jukwaa la kukoleza pia majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine, ili dunia iwe ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.








All the contents on this site are copyrighted ©.