Baba Mtakatifu Francisko anaungana na ndugu, jamaa na wote waliopatwa na maafa kutokana
na ajali ya treni iliyotokea huko Santiago de Compostella, Hispania, siku ya Jumatano,
tarehe 24 Julai 2013 na kusababisha watu 77 kufariki dunia na wengine 140 kupata majeraha
makubwa.
Hayo yamesemwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa vatican
alipokuwa anazungumza na jopo la waandishi wa habari lililoko kwenye msafara wa Baba
Mtakatifu Francisko nchini Brazil. Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kurudi tena nchini
Brazil kunako mwaka 2017 wakati wa Jubilee ya miaka 300 tangu Sanam ya Bikira Maria
Mkingiwa Dhambi ya Asili ilipoibuliwa kutoka katika mto Paraiba.
Na Mwaka
2017, Madhabahu ya Fatima yatakuwa yanafanya Jubilee ya Miaka 100, itakuwa ni fursa
kwa Baba Mtakatifu kutembelea maeneo haya.
Baba Mtakatifu wakati wa chakula
cha mchana kwenye Seminari ya Kristo Mchungaji mwema, alipata fursa ya kusalimiana
na Jumuiya pamoja na wafanyakazi; amewashukuru na kuwapongeza wapishi kwa kazi kubwa
waliyoifanya na wengi wao wamefanikiwa kupata picha ya kumbu kumbu kwani hapa kulikuwa
hakuna haraka anasema Padre Lombardi. Baba Mtakatifu ametumia muda wake wa mapumziko
kwa ajili ya kusalimiana na kuzungumza na watu mbali mbali waliokuwepo Seminarini
hapo.