Kanisa ni kijana kutokana na ujana wa vijana wenyewe! Maajabu ya Mungu!
Mheshimiwa Padre Raymond Saba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania limetuma ujumbe "mnene" kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko
Rio de Janeiro, Brazil.
Padre Saba
katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, vijana wanapaswa kupambua dhamana
na wajibu wao ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla kwamba, wao ni nguzo, jeuri na mboni
ya jicho la Kanisa. Vijana wanapaswa kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu kwa njia
ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu. Ujana ni "nongwa", lakini katika ujana
kuna mang'amuzi makubwa, nguvu nyingi zinazopaswa kutumia vyema kwa ajili ya mafao
na maendeleo ya wengi kiroho na kimwili na wala si kwa ajili ya kubomoa! Ujana ni
kipindi kilichojaa ubunifu, unaoweza kutumika pia katika azma ya Uinjilishaji wa kina.
Vijana wautumie ujana wao kuwashirikisha na kushirikishana tunu msingi za
maisha ya Kiinjili; wajiimarishe na kuwaimarisha vijana wenzao katika misingi ya imani,
maadili na utu wema. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alipenda kusema
kwamba, Kanisa ni kijana kutokana na ujana wa vijana wenyewe anasema Padre Saba kwamba,
haya ndiyo maajabu ya Mungu kwa waja wake.
Vijana wanahamasishwa kuona ari
na nguvu iliyoko ndani mwao kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Kanisa ambalo limejengwa
kutokana na msingi thabiti wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo litaendelea kubaki
ni kijana. Vijana na ujana wao ni tunu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa.
Papa
Francisko anataka kuwaimarisha vijana, ili nao kwa wakati ufaao waweze kuwaimarisha
na kuwainjilisha vijana wenzao, kwani wanatumwa kwenda ulimwenguni kote kuwafanya
mataifa yote kuwa ni wanafunzi, kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya 28 ya
Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.