Kanisa linahamasishwa kumwilisha imani katika matendo!
Mama Kanisa anachangamotishwa na Kristo mwenyewe kuhakikisha kwamba, anamwilisha dhana
ya Msamaria mwema katika maisha na utume wake kama njia ya kupambana na vitendo vinavyosababisha
uvunjifu wa misingi ya haki na amani, kwa kuonesha umuhimu wa Fumbo la Msalaba.
Uinjilishaji
daima unakwenda sanjari na mikakati ya maendeleo endelevu inayopania kumhudumia mtu
mzima: kiroho na kimwili, daima heshima na utu wa binadamu vikipewa kipaumbele cha
kwanza. Huu ndio ushuhuda unaoneshwa na Hospitali ya Mtakatifu Francisko iliyofunguliwa
na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Siku a Vijana Duniani kwa Mwaka
2013. Ni hospitali inayotoa huduma kwa vijana walioathirika na matumizi haramu ya
dawa za kulevya.
Vijana watakaobahatika kupona na kurudi katika maisha ya
kawaida, kwa hakika watakuwa ni matunda ya Uinjilishaji wa kina, unaoliwezesha Kanisa
kuwamegea watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kama kielelezo
makini cha umoja na mshikamano wa kidugu na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Hizi ni jitihada za Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika
matendo ya huruma, kielelezo makini cha ushuhuda wa imani katika matendo! Ni mwaliko
wa kuendeleza ile huruma ya Mwenyezi Mungu kwa wote wanamkimbilia wakitaka kuonja
tena upendo wake baada ya kuathirika kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Hii
ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Oran Joao Tempesta, Jumatano tarehe
24 Julai 2013 mbele ya Baba Mtakatifu Francisko katika ufunguzi wa Hospitali ya Mtakatifu
Francisko, maalum kwa ajili ya wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili; vijana wanaojitahidi
kujiondoa kutoka katika utumwa na mnyororo wa matumizi haramu ya dawa za kulevya.
Ujenzi wa Hospitali hii ni matunda ya ushirikiano kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia na Kanisa Katoliki nchini Brazil.
Vijana wengi waliotoa ushuhuda wao
wanasema, uchaguzi wa jina la Francisko uliofanywa na Baba Mtakatifu mara tu baada
ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa ni kielelezo makini cha mradi wa maisha unaopaswa
kufanyiwa kazi, kama alivyofanya Mtakatifu Francisko aliyejitoa bila kujibakiza kwa
ajili ya maskini na wagonjwa wa ukoma kwa nyakati zake.
Ni mwaliko wa kuganga
miili ya watu na kuponya roho zao kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Hata leo hii,
Baba Mtakatifu anaendelea kuchangamotishwa na Kristo kwa njia ya maneno ya Mtakatifu
Francisko wa Assis, Jenga Kanisa langu! Hospitali hii ni shule ya utakatifu wa maisha,
inayowaonjesha watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo. Hii ndiyo hamu ya Baba
Mtakatifu Francisko kuona kwamba, Kanisa linajitosa kimaso maso kwa ajili ya huduma
kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Matumizi haramu ya
dawa za kulevya ni janga kubwa nchini Brazil ambayo kwa sasa inaongoza kwa kuwa na
watumiaji wengi wa dawa za kulevya. Kumbe, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko katika
Hospitali hii umekuwa ni tukio ambalo linaacha chapa ya kudumu kwa Brazil, lakini
kwa vijana wanaohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kutambua madhara ya
matumizi haramu ya dawa za kulevya il kamwe wasijitumbukize wala kuwatumbukiza wengine
huko!