Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwasili nchini Brazil na kupata mapokezi makubwa,
Jumanne alipumzika kidogo, huku akikusanya nguvu tayari kuanza pilika pilika pilika
za Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Askofu mkuu Oran Joao Tempesta
wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro, ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajioli
ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani.
Baba Mtakatifu
Francisko katika ujumbe wake kwa vijana wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho haya anawaambia
kwamba, Yesu Kristo ana matumaini makubwa na vijana na anapenda kuwakabidhi utume
wake akisema, basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi.
Wakati
huu kuna Maaskofu 250 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoendesha Katekesi ya
kina kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Vijana: Mada kuu zinazoongoza Katekesi hizi ni:
"kiu ya matumaini, kiu ya Mungu"; "Jinsi ya kuwa mfuasi wa Yesu"; Iweni Wamissionari,
nendeni". Katekesi hizi zinaendeshwa katika maeneo zaidi ya 300 yaliyotawanyika mjini
Rio de Janeiro.