2013-07-24 16:00:22

Vijana wanachangamotishwa kuwa ni wamissionari katika mchakato wa Uinjilishaji mpya!


Askofu mkuu Oran Joao Tempesta wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro, Jumanne jioni, alifungua rasmi kwa Ibada ya Misa Takatifu kama mwanzo wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, kwenye ufuko wa Copacabana. Vijana wakiwa na ari na shauku kubwa waliupokea Msalaba wa Vijana, uliokuwa umebebwa na wawakilishi wa vijana kutoka Mabara yote matano.

Katika Ibada hii, vijana wamesali na kuwaombea vijana wenzao wasiokuwa na fursa ya kazi, vijana waliofariki dunia wakiwa kwenye ukumbi wa muziki nchini Brazil, watoto wanaopoteza maisha yao na wale vijana waliofariki dunia wakiwa njiani kwenda Rio kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Askofu mkuu Joao Tempesta amewataka vijana kuwa ni Wamissionari miongoni mwa vijana wenzao kwa kutambua kwamba, wao ni kati ya makundi yanayopewa umuhimu wa pekee kabisa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Uwepo wao nchini Brazil ni mwaliko wa kutaka kushirikishana na kumegeana imani na furaha ya kuwa ni Wafuasi na Wamissionari wanaotumwa kumtangaza Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili. Vijana ni sura inayoonesha ujana wa Kanisa mintarafu Injili ya Kristo.

Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha vijana kuwa ni wadau wakuu wa Uinjilsihaji Mpya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Dunia inawahitaji vijana moto moto, tayari kuwasha moto wa imani, upendo na matumaini na mshikamano wa dhati. Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele yao hata mara baada ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayofanyika Amerika ya Kusini baada ya miaka 26, kwa kumpokea na kumkirimia Papa Francisko, kutoka Amerika ya Kusini.

Kanisa linawashukuru vijana kwa kuonesha moyo wa upendo kwa jirani zao lakini zaidi kwa Kristo ambaye ni Bwana na Mwalimu makini. Vijana watambue kwamba, wanatumwa na Mama Kanisa kuinjilisha hadi miisho ya dunia kwa kuwaonjesha jirani zao matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka.







All the contents on this site are copyrighted ©.