Picha ya Bikira Maria wa Aparecida iwe ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii!
Kardinali Damasceno Assis, Askofu mkuu wa Aparecida katika hotuba yake ya utangulizi
kabla ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko,
hapo tarehe 24 Julai 2013, ameelezea historia fupi ya Madhabahu ya Bikira Maria wa
Aparecida, tangu mwaka 1717.
Mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamefika
na kutembelea Madhabahu haya, wakiwa wanaongoza na matumaini. Hija ya Baba Mtakatifu
mahali hapo ni fursa ya kuwaimarisha ndugu zake katika ukweli wa imani na upendo katika
hija ya utakatifu wa maisha.
Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida ni kielelezo
na utambulisho muhimu wa Brazil, ndiyo maana Baba Mtakatifu amependa kuweka Maadhimisho
ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira
Maria wa Aparecida, ili awaimarishe vijana katika imani, matumaini na mapendo thabiti
kwa Yesu, daima wakiwa tayari kumwilisha ujumbe wa Yesu, unaowachangamotisha kwenda
ulimwenguni kote kuwafanya mataifa yote kuwa ni wanafunzi.
Madhabahu haya
yamekwisha wapokea Mwenyeheri Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa
kumi na sita, na leo hii, Papa Francisko. Kardinali Damasceno Assis amemzawadia Baba
Mtakatifu Picha ya Bikira Maria wa Aparecida, inayoonesha mateso na mahangaiko ya
maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, hasa wananchi wa Brazil ambao
wana asili ya kiafrika. Hii ni Jamii ambayo imeshuhudia pia ubaguzi na nyanyaso katika
maisha yao.
Hii ni changamoto kwa Kanisa Katoliki nchini Brazil kujikita katika
dhamana ya Uinjilishaji mpya, kwa kuonesha mshikamano na maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii; wakiwa huru, waweze kuhudumia kwa ukamilifu zaidi. Kanisa nchini
Brazil linamtakia kheri, baraka na mafanikio katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu
Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Wanamwombea ili aweze kuwa shahidi
mwaminifu katika kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili; imara katika imani anapokumbana
na changamoto za maisha, daima akitegemea ulinzi na usimamizi wa Mwenyezi Mungu na
maombezi ya Bikira Maria wa Aparecida.