2013-07-24 16:35:15

Papa ajiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Aparecida!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza rasmi Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida, akimwomba amsindikize katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya imani, kila jambo linawezekana mbele ya Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu ameyaweka maisha yake mikononi mwa Bikira Maria wa Aparecida pamoja na Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo, ili waweze kufanya hija ya maisha ya imani pamoja naye, akimpeleka mbele ya Mwenyezi Mungu, ili awekwe wakfu. Amewaweka vijana wanaohudhuria Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Aparecida, ili ari, mwamko na nguvu walizo nazo ziweze kutumika kwa ajili huduma ya maisha na binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni, amemwomba Bikira Maria endelee kuwapokea mahujaji wanaofika Madhabahuni hapo; awasindikize wanapotekeleza wajibu wao mkubwa kama Familia ya Mungu; lakini zaidi, awasaidie kubeba Msalaba pale unapowaelemea, daima akiwatia shime katika imani na matumaini.

Mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko alisali tena kwa Bikira Maria wa Aparecida, akiwaombea kwa namna ya pekee, wananchi wa Brazil ili waonje huruma na upendo wake. Amejiweka wakfu ili awaze, aseme, atende na kumpenda kuliko kitu kingine chochote katika maisha yake. Anamwomba Bikira Maria aweze kumlinda na kumkinga; amkirimie mahitaji yake msingi: kiroho na kimwili, hasa zaidi wakati wa kufa.

Amemwomba Bikira Maria wa Aparecida amwombee katika mapungufu yake ya kibinadamu, ili aweze kuwa mwaminifu katika utume wake, kwa kumsifu, kumpenda na kumshukuru.







All the contents on this site are copyrighted ©.