Hali ya wakimbizi eneo la Maziwa Makuu bado si shwari!
Askofu mkuu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania katika mahojiano na maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba,
Tanzania ambayo imekuwa ikitoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za
nchi za Maziwa Makuu inakabiliwa na changamoto kadhaa. Ukweli ni kwamba, kwa sasa
kuna wakimbizi wachache wanaoishi nchini Tanzania.
Lakini hapa
kinachoangaliwa anasema Askofu mkuu Ruzoka, si idadi ya watu, bali kila mtu anapaswa
kuangaliwa kama mtu binafsi anayetafuta hifadhi, usalama na nafuu ya maisha kutokana
na sababu mbali mbali nchini mwake zinazomlazimisha kuyahama makazi yake. Tangu kunako
mwaka 1959, Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka Rwanda na kunako
mwaka 1972 ikaanza pia kupokea wakimbizi kutoka Burundi nab ado kuna idadi ndogo ya
wakimbizi wanaoishi ndani ya mipaka ya Tanzania.
Kumekuwepo na mchakato kwa
wakimbizi kuamua kurudi makwao au kubaki Tanzania na kupewa uraia wa Tanzania. Hofu
bado imetanda kwa wale wakimbizi waliojiandikisha kuomba uraia wa Tanzania, kwani
hadi sasa bado hawajapata jibu muafaka na hivyo hawana habari kwa kile kinachoendelea
kwa sasa. Kigoma kuna wakimbizi kutoka DRC wanaoishi kwenye Kambi ya wakimbizi ya
Nyalugusu, wote hawa wanatafuta hifadhi na usalama wa maisha yao na kwamba, Serikali
ya Tanzania inaendelea kulishughulikia tatizo hili.
Kanisa limekuwa mstari
wa mbele kuwahudumia wakimbizi kwa hali na mali pamoja na kuwapatia huduma za kiroho
kwa wale wakimbizi wanaoishi Tabora na Kigoma. Tangu mwaka 1973 maeneo yao yamekuwa
ni Parokia, utume ambao unaendelezwa kwa sasa.
Askofu mkuu Ruzoka anasema,
hali ya wakimbizi kwenye nchi za Maziwa Makuu bado ni tete kutokana na mgogoro wa
kisiasa na vita inayoendelea huko Mashariki mwa DRC kati ya Jeshi la Serikali na M23.
Hivi karibuni, nchi za SADC zimeamua kupeleka vikosi vya ulinzi na usalama ili kusaidia
mchakato wa kuleta amani nchini DRC. Migogoro ya kisiasa na vita huko DRC ni mambo
ambayo yataendelea kuzalisha wimbi kubwa la wakimbizi.
Askofu mkuu Paul Ruzoka
ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi
anasema, katika mkutano wao uliohitimishwa hivi karibuni mjini Vatican, Baba Mtakatifu
Francisko aliwakumbusha kwamba, suala la wakimbizi na wahamiaji ni tete na kwamba,
Kanisa halina budi kuendelea kujishughulisha zaidi na watu wanaoishi katika mazingira
hatarishi: kwa kuwatia moyo, kuwahudumia pamoja na kuwajengea misingi ya: haki, amani,
upatanisho na utulivu.
Kanisa liendeshe shughuli zake kwa njia ya ushawishi
kwa kuhakikisha kwamba, Serikali inawajali raia wake na wale wanakimbilia usalama
na amani katika mipaka yake, kwani hakuna maendeleo ya kweli na endelevu pasi ya haki
na amani.