Vijana msiwe ni bendera kufuata upepo, mtalizwa na wajanja!
Padre Beno Michael Kikudo kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam anawaambia vijana wanaohudhuria
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro kwamba, hili
ni tukio muhimu sana katika maisha yao ya kiroho na ustawi wa maendeleo yaokwa siku
za usoni. Hiki si kipindi cha utalii na kuvinjari mazingira ya Brazil ambayo inasifika
sana kwa kutandaza kabumbu duniani na yenye vivutio vingi vya kitalii!
Vijana watambue
kwamba, wamepewa fursa na Mama Kanisa ya kufanya hija ya maisha yao ya kiroho, inayowawezesha
kukutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia; changamoto ya kutuliza mawazo,
maneno na matendo yao, ili waweze kufaidika na yale ambayo Mama Kanisa amewaandalia.
Vijana wawe makini katika sala, katekesi, maadhimisho ya Ibada mbali mbali, ili kufanikisha
malengo ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, wakiwa tayari kuzijibia changamoto
za ujana katika maisha yao ya kila siku.
Padre Kikudo anasema, vijana wa kitanzania
maarufu kama "vijana wa bongo country" wanakabiliana na changamoto zile zile kama
ilivyo kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa vijana ambao hawakupata
fursa ya kwenda Brazil, wahamasike kuungana na vijana wenzao kadiri ya nafasi na fursa
zilizopo ili wasipitwe kamwe na yale yanayojiri katika Maadhimisho haya.
Kila
kijana anachangamotishwa na Mama Kanisa kutambua dhamana na wajibu wake ndani ya Jamii,
tayari kuutekeleza kwa moyo mkuu na ari kubwa zaidi. Kijana anapaswa kuwa na msimamo
thabiti katika maisha na kamwe asiwe ni bendera kufuata upepo kwani anaweza "kulizwa"
na wajanja katika maisha!