2013-07-23 09:27:04

Kardinali Pimenta azikwa, nchini India


Kardinali Simon Ignatius Pimenta, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Bombay aliyefariki dunia hivi karibuni nchini India akiwa na umri wa miaka 93 anazikwa, Jumanne, tarehe 23 Julai 2013 mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Jina takatifu, Jimbo kuu la Bombay. Waamini na watu wenye mapenzi mema wamepata nafasi ya kutoa salam na heshima zao za mwisho.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pimenta alizaliwa kunako tarehe 1 Machi 1920. Mara baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 21 Desemba 1949. Tarehe 5 Juni 1971 Papa Paulo VI akamteua kuwa Askofu na kuwekwa wakfu hapo tarehe 29 Juni 1971. Tarehe 26 Februari 1977 aliteuliwa kuwa ni Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Bombay, India.

Mwenyeheri Yohane Paulo II, tarehe 28 Juni 1988 akamteuwa kuwa Kardinali na baadaye tarehe 8 Novemba 1996 akang'atuka kutoka madarakani kadiri ya sheria za Kanisa. Amewahi kuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki India katika kipindi cha Mwaka 1982 hadi mwaka 1988 na Mwaka 1994 hadi mwaka 1996. Amefariki dunia hapo tarehe 19 Julai 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.