Brazil inatambua mchango wa Papa Francisko katika kutetea haki jamii!
Rais Dilma Rouseff wa Brazil, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa kwanza
wa Mtakatifu Petro kutoka Amerika ya Kusini anayetembelea Brazil katika Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Vijana wa Brazil wapatao millioni 50 wanaungana
na vijana wengine kutoka sehemu mbali mbali za dunia kumpokea Baba Mtakatifu kwa moyo
wa ukarimu.
Brazil inamtambua Papa kuwa ni kiongozi wa kiroho, mtu makini katika
masuala yanayogusa haki jamii na adui mkubwa wa ubaguzi kati ya watu na utandawazi
unaowafanya watu kutoguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine. Ni kiongozi
anayependa kutetea wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kama inavyojionesha
katika jina alilolichagua yaani Francisko.
Rais Dilma Rouseff anasema, Brazil
imepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini bado kuna mambo mengi yanayopaswa kuboreshwa.
Njaa na kiu ya haki ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Hivi
ndivyo ilivyojionesha katika maandamano na vurugu za kisiasa zilizojitokeza hivi karibuni.
Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa nchini Brazil kwa pamoja wanapania
kuvuka vikwazo vya myumbo wa uchumi kimataifa kwa kutoa nafuu ya maisha kwa maelfu
ya watu wasiokuwa na fursa za ajira na maskini. Lengo ni kuondokana na woga usiokuwa
na msingi pamoja na makosa ya jinai.
Brazil ni nchi ya watu wenye imani zao,
lakini wanakabiliana na changamoto nyingi kama inavyojionesha nchini humo, kwani kumekuwepo
na maandamano kupinga sera na mikakati ya Serikali; yote haya yanaonesha utashi wa
wananchi wa Brazil kutaka kuwa na maisha bora zaidi. Vijana wa Brazil wamepania kufanya
maboresho ya kina katika maisha yao, jambo muhimu sana hata katika Maadhimisho ya
Siku ya Vijana Duniani.
Rais Dilma Roussef anasema vijana wana ari, moyo na
furaha; wanaonesha ujasiri na mwamko wa kutaka kupata fursa ya kugundua tunu msingi
za maisha. Ni matumaini yake kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani nchini
Brazil yataleta matunda yanayokusudiwa kwa vijana nchini Brazil na kutoka sehemu mbali
mbali za dunia.