Biashara haramu ya binadamu ni uvunjifu wa msingi ya utu na heshima ya binadamu
Viongozi wa Makanisa nchini Ufilippini wanaendelea kushikamana kupinga biashara haramu
ya binadamu inayoendelea kushamiri nchini humo siku hadi siku. Wanaitaka Serikali
ya Ufilippini pamoja na Serikali za nchi nyingi za Kiasia, kuhakikisha kwamba, zinachukua
hatua za kisheria dhidi ya biashara haramu ya binadamu, hali ambayo inaendelea kusababisha
uvunjifu wa misingi ya utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa
Mungu.
Hayo yamebainishwa
hivi karibuni na Askofu msaidizi Broderick Pabillo wa Jimbo kuu la Manila. Anasema,
biashara haramu ya binadamu ni tatizo linaloendelea kuota mizizi nchini humo, kumbe,
kuna haja kwa Jamii ikisaidiana na Serikali kuweka mikakati ya kupambana na biashara
hii inayowatumbukiza watoto na wasichana katika utumwa mamboleo. Makanisa hayawezi
kukaa kimya huku utu na heshima ya binadamu vikiendelea kudhalilishwa na watu wachache
wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka kwa kutumia mgongo wa wanyonge ndani
ya Jamii.
Biashara haramu ya binadamu ni matokeo ya umaskini, rushwa na uvunjaji
wa sheria unaofanywa na baadhi ya watu kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa
ajili ya mafao ya binafsi. Ni biashara ambato inawatumbukiza watoto na wasichana katika
biashara ya ukahaba na kwamba, Serikali bado inaendelea kulifumbia macho tatizo hili
licha ya taarifa za Jumuiya ya Kimataifa iliyochapishwa kunako mwaka 2012 kuonesha
kwamba, waathirika wa biashara hii hawana hifadhi yoyote ile!
Wahusika wa
biashara haramu ya binadamu wanaendelea kula “kuku kwa mrija” wakati ambapo utu na
heshima ya binadamu inadhalilishwa na kutezwa. Wahusika wameshindwa kufikishwa kwenye
vyombo vya kisheria ili sheria iweze kuchukua mkondo wake! Biashara haramu ya binadamu
inalenga pia kutoa ajira kwa ujira mdogo kwa makampuni makubwa ya kimataifa yanayoendelea
kuwekeza Barani Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani.
Takwimu zinaonesha
kwamba, idadi ya wananchi kutoka nchini Ufilippini imefikia walau millioni kumi! Rais
Benigno Aquino wa Ufilippini, ameipokea changamoto hii kwa mwelekeo chanya na kuahidi
kwamba ataifanyia kazi, ili kudhibiti biashara haramu ya binadamu.