2013-07-22 11:29:59

Sala na kazi: Ora et Labora: ni chanda na pete!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita, tarehe 21 Julai 2013, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alizungumzia kuhusu umuhimu wa sala na kazi kama kielelezo cha maisha ya Mkristo, kama ilivyojionesha wakati Yesu alipotembelea Familia ya Maria na Martha, dada zake Lazaro.

Sala na kazi ni chanda na pete na wala hakuna msigano wa aina yoyote ile; ni mambo yanayopaswa kumwilishwa kikamilifu katika maisha ya wafuasi wa Kristo. Yesu anamwonya Martha aliyejitaabisha mno kwa mambo ya kidunia na kwamba, alihitaji pia kusikiliza Neno la Mungu, kama alivyokuwa anafanya dada yake Maria, huu ndio mwelekeo sahihi kwa mfuasi wa Kristo. Wakristo wajibidishe kuwahudumia ndugu zao wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, huku wakiendelea kujitajirisha katika maisha yao ya kiroho kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, kwa kiongozi yeyote wa Kanisa anayeelemewa mno na shughuli za kichungaji, akasahau kujibidisha katika sala, kuna hatari kwamba, mtu kama huyu anajitafuta na kujihudumia mwenyewe. Yesu Kristo anapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya sala na huduma kwa jirani. Waamini wajenge utamaduni wa kuzungumza na Yesu kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; mambo ambayo yanajenga na kuimarisha uhusiano wa karibu na Kristo, kama alivyokazia Mtakatifu Benedikto, Abate, Ora et Labora!

Huduma kwa maskini na wahitaji ipate chimbuko lake kutoka kwa Kristo kwani huduma hii pia inaweza kumpeleka mwamini kwa Kristo. Ni mwaliko kwa waamini kumwomba Bikira Maria, Mama aliyefaulu kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kuhudumia awafundishe kutafakari Neno la Mungu na kusali kwa uaminifu, daima wakiwa makini kuona na kuguswa na shida za jirani zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.