2013-07-22 10:11:43

Onesheni moyo wa upendo na ukarimu kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii


Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini, hivi karibuni, akiwa kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na kati, CUEA, katika Maadhimisho ya mkutano mkuu wa wataalam wa masuala ya Umissionari Kimataifa, amewataka Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa ukarimu kwa wageni, wenye shida na mahangaiko mbali mbali ya maisha, lakini hasa zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Umaskini, athari za myumbo wa uchumi kimataifa, maafa na majanga asilia, vita na migogoro na kinzani za kisiasa, kijamii pamoja na madhulumu ya kidini ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia kuwafanya watu kuyakimbia makazi na nchi zao, kiasi hata cha kujikuta wakiwa wanatanga tanga kutafuta hifadhi ya maisha.

Dhamana ya uinjilishaji Mpya inatoa changamoto kwa Kanisa kuona jinsi ya kutumia kila fursa na nafasi inayopatikana kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Takwimu za Kimataifa kwa Mwaka 2012 zinaonesha kwamba, asilimia 44% ya wahamiaji, wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Idadi kubwa ya watoto hawa wanapatikana Afrika ya Kaskazini, ambako katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na machafuko ya kisiasa na vita. Idadi hii ni kidogo kwa nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki. Tatizo la wakimbizi na wahamiaji linapaswa kushughulikiwa kikamilifu.

Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kuonesha moyo wa ukarimu kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kwani Ukarimu ni sehemu ya utambulisho na vinasaba vya Kanisa tangu mwanzo.

Kardinali Tagle anasema, kuna idadi kubwa ya wananchi kutoka Ufilippini wamehamia katika nchi mbali mbali duniani ili kutafuta malisho bora zaidi pamoja na kuendelea kuzitegemeza familia zao. Lakini mwelekeo huu una madhara yake kwani familia nyingi ambazo zina wazazi wanaofanya kazi nje ya nchi zimejikuta kuwa zinatumia vibaya fedha na sadaka inayotolewa na ndugu zao kwa kujinyima. Matokeo yake, familia hizi zimejitumbukiza katika anasa.

Kumbe, kuna haja ya kuendelea Kuinjilisha, kwa kuonesha ukarimu na kuwajali wengine, watu watambue sadaka na majitoleo ya ndugu zao wanaojinyima kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchi zao asilia. Wahamiaji na wakimbizi ni watu wanaobeba ndani mwao amana za maisha na tunu msingi za imani na utu wema. Hawa wamekuwa ni mihimili mikuu ya Makanisa wanapokuwa ugenini, kama inavyojionesha kwenye Falme za Kiarabu na huko Mashariki ya Kati.

Wahamiaji na wageni hawa wanabeba ndani hazina ya imani wanayowashirikisha wenyeji wao wanapokuwa ugenini. Uinjilishaji mpya, uone matatizo, changamoto na fursa zinazojitokeza kama njia ya kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Leo hii Yesu bado anaendeleza majadiliano ya kina katika maisha ya kila mfuasi wake kama alivyofanya na yule Mwanamke Msamaria. Kila mwamini awe tayari kutoa na kupokea amana za imani kutoka kwa jirani yake. Kila mtu hata katika umaskini wake, anayo amana ambayo anaweza kuchangia au kuwashirikisha ndugu zake katika Kristo.








All the contents on this site are copyrighted ©.