2013-07-22 11:11:55

"Naomba mnisindikize kwa sala, imani, toba na wongofu wa ndani wakati wa Maadhimisho ya Juma la Vijana Duniani kwa Mwaka 2013"


Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 22 Julai 2013 asubuhi, ameanza hija yake ya kwanza ya kimataifa nchini Brazil, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, inayoongozwa na kauli mbiu "Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi. Baba Mtakatifu na ujumbe wake, anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Antonio Carlos Jobim alasiri kwa masaa ya Brazil, sawa na saa 4:00 kwa saa za Afrika Mashariki.

Akiwa kwenye Uwanja wa ndege mjini Roma, Baba Mtakatifu amesindikizwa na Waziri mkuu wa Italia Bwana Enrico Letta, viongozi wa Kanisa na Serikali ya Italia.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, Baba Mtakatifu aliwashukuru waamini na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwaomba wamsindikize kwa njia ya sala, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Juma la Vijana Kimataifa. Vijana ndio wadau wakuu katika Maadhimisho haya, wana shauku kubwa ya kusikiliza Yesu anawaambia nini katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana wengine wote ambao hawakupata bahati ya kwenda Brazil, kuendelea kutafakari ujumbe wa Yesu katika maisha yao, tayari kujitosa kimaso maso kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu aliiweka safari na maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani chini ya usimamizi na maombezi ya Bikira Maria anayeheshimiwa sana nchini Brazil.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi iliyopita majira ya jioni, alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko mjini Roma na huko alipokelewa na viongozi wakuu wa Kanisa hili. Akaenda moja kwa moja kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, akiwa amezungukwa na Mapadre wa Shirika la Wadominikani wanaohudumia Kanisa hapo.

Amesali katika hali ya ukimya kwa takribani nusu saa, akaweka shada la maua na kuwasha mshumaa uliokuwepo mahali hapo. Tukio hili limeshuhudiwa na waamini pamoja na mahujaji waliokuwepo Kanisa hapo kwani Baba Mtakatifu Francisko alikwenda Kanisani hapo bila ya maandalizi maalum. Amewaalika waamini waliobahatika kumsikiliza mara baada ya kuhitimisha sala zake kumsindikiza kwa njia ya sala, imani lakini zaidi kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Baadaye, Baba Mtakatifu alirejea tena mjini Vatican, kuendelea na maandalizi ya Jumapili na hatimaye, hija ya kichungaji nchini Brazil.








All the contents on this site are copyrighted ©.