2013-07-22 09:39:09

Mwaliko kwa vijana kufuata nyayo za Bwana!


Maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa Mwaka 2013 yanapambwa pia na Onesho la picha mbali mbali linaoongozwa na kauli mbiu “kufuata nyayo za Bwana” lililoandaliwa na Taasisi ya Yohane Paulo II kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Walei. Onesho hili limefunguliwa hapo tarehe 9 Julai 2013 na linatarajiwa kufungwa rasmi hapo tarehe 12 Oktoba 2013, kwenye Jumba la Makumbusho ya Taifa mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Onesho hili la picha ni mwendelezo wa kazi za wasanii maarufu kutoka sehemu mbali mbali za dunia zilizopangwa katika makundi makuu manne: Kristo, njia ya wokovu; Wito na Utume wa Wafuasi wa Yesu; Bikira Maria njia inayowapeleka waamini kwa Kristo na mwishoni ni sehemu ya watakatifu, ambao wanaendelea kutoa changamoto kwa vijana kwenda kuwafanya wote kuwa ni wanafunzi wa Yesu kwa njia ya mifano na ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu.

Kristo, njia, ukweli na uzima ni mfululizo wa kazi za wasanii zinazoonesha kwa muhtasari kuhusu: maisha ya Yesu: mateso, kifo na ufufuko wake. Kwa namna ya pekee, Mtume Toma anaoneshwa kuwa ni kati ya wale wafuasi wa Yesu waliokuwa na imani haba hadi pale alipogusa madonda matakatifu, hapo akapigwa na bumbuwazi kiasi cha kumkiri Yesu kuwa ni Mungu na Bwana.

Yule mwanamke aliyefumaniwa akizini na baadaye akaonja huruma na upendo wa Yesu, imeoneshwa, bila kusahau ile picha ya Msamaria mwema, mwaliko kwa kila mwamini kuwa ni Msamaria mwema kwa jirani yake, lakini zaidi kwa wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Onesho hili la picha ni kielelezo makini cha imani ya watu mbali mbali, walioishuhudia kwa njia ya picha ambazo zimeacha mvuto na mguso mkubwa katika historia ya binadamu. Ni picha ambazo zimechaguliwa kwa umakini mkubwa ili kuwasaidia waamini lakini kwa namna ya pekee vijana wanaohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 kuchangamkia ushuhuda wa maisha. Sanda Takatifu ya Torino, itaoneshwa pia katika mfumo wa picha.

Haya ni maonesho kwa wale ambao wamebahatika kufika Rio de Janeiro, kujitahidi kuchungulia kwani kila kitu kilichopangwa kwa ajili ya Maadhimisho haya, kinapania kwa namna ya pekee kuwaimarisha vijana katika Uinjilishaji mpya na ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.