Masista wa Ivrea waanza Maadhimisho ya Jubilee za maisha ya kitawa!
Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi
yake kwa ajili ya Kristo ndiye atakayeisalimisha. Huu ni muhtsari wa ujumbe wa Yesu
kwa wafuasi wake wa nyakati zote. Mtu kuiangamiza nafsi yake kwa ajili ya Yesu kuna
maana kuu mbili: kuiungamana imani au kusimama kidete kutetea ukweli!
Mashahidi
na waungama imani ni wale ambao wameyamimina maisha yao kwa ajili ya Yesu Kristo.
Katika kipindi cha miaka elfu mbili ya Ukristo kuna Wakristo wengi waliopoteza maisha
yao ikilinganishwa na idadi ya Wakristo wa Kanisa la Mwanzo. Ni mashahidi waliothubutu
kujitoa kimasomaso ili kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.
Ni
tafakari iliyotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko na kuendelea kusema
kwamba, Mashahidi wa Injili wanaojionesha kila siku ya maisha, wakati wakitekeleza
dhamana na wajibu wao kwa Kanisa, Familia na Jamii inayowazunguka.
Hawa ni
Makleri, Watawa, Wazazi na Walezi pamoja na vijana. Ni watu wanaoonesha sadaka ya
maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake; wanajitahidi kurithisha imani na mafao kwa watoto
wao ni vijana wanaojitoa kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji zaidi.
Baba Mtakatifu
Francisko anasema, hata hawa ni mashahidi wa Kristo katika uhalisia wa maisha ya kila
siku. Kuna Wakristo na watu wengine katika Jamii ambao wameyamimina maisha yao kwa
ajili ya kulinda na kutetea ukweli, kwani Kristo mwenyewe amesema, Yeye ndiye ukweli
na uzima.
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Shirika la Masista wa Upendo
wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili la Ivrea, linawaalika watawa wake kuwa waaminifu
kwa wito na maisha yao ya kitawa, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu
katika ahadi zake.
Kutokana na ukweli huu, Shirika hili linawasherehekea watawa
wake waliotimiza miaka 15, 25 na 35 ya maisha ya kitawa, kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu
utenzi wa sifa na shukrani, huku wakiyaelekeza macho yao kwa Bikira Maria, Mama aliyejitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake.
Mheshimiwa
Sr. Palma Porro, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa
dhambi ya Asili la Ivrea anasema kwamba, kuanzia tarehe 21 hadi 28 Julai 2013, Masista
23 kutoka sehemu mbali mbali za dunia watakusanyika mjini Roma ili kujinoa katika
tasaufi ya maisha yao ya kiroho. Kuanzia tarehe 29 Julai hadi tarehe 16 Agosti 2013
watakuwa Andrate, Kaskazini mwa Italia kushiriki katika kozi ya majiundo endelevu
na kilele cha Jubilee hizi ni hapo tarehe 15 Agosti 2013, Siku kuu ya Bikira Maria
Kupalizwa mbinguni.
Maadhimisho haya yatafanyika kwenye Kanisa la Bikira Maria
wa Miujiza, Jimboni Ivrea. Huu utakuwa ni muda muafaka wa kusali, kutafakari kwa kina
Neno la Mungu, pamoja na kushirikishana, furaha, majonzi na mang’amuzi ya maisha ya
kitawa.
Masista wa Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili wa Ivrea,
watakuwa wanasindikizwa na Mwenyeheri Mama Antonia Maria Verna, mwanamke wa shoka,
aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani.