Caritas Hong Kong katika huduma ya watu: kiroho na kimwili!
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Hong Kong, hivi karibuni limeadhimisha
kumbu kumbu ya miaka 60 tangu lilipozinduliwa na hivyo kuwa kwelini kitovu cha majiundo
na mikakati ya maendeleo endelevu. Caritas Hong Kong ni kati ya Mashirika makubwa
ya Misaada ya Kanisa Katoliki katika ngazi ya Kijimbo.
Lina jumla
ya wanachama elfu kumi wanaojitolea sehemu mbali mbali Barani Asia na kwamba, lina
endesha miradi mikubwa nchini Japan, India, Vietnam, New Zealand, Australia na China.
Ni maneno ya Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu
misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, baada ya kurejea mjini Vatican kutoka Hong Kong
alikokuwa anahudhuria Maadhimisho ya Miaka 60 ya Caritas Hong Kong. Akiwa nchini humo,
aliwasilisha pia salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, anayetambua
na kuthamini uwepo wa Kanisa Katoliki Barani Asia na kwa namna ya pekee kabisa nchini
China. Hii inaonesha kwamba, Mama Kanisa anawapenda watoto wake wote bila ubaguzi
wa aina yoyote ile!
Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 60 ya Caritas Hong
Kong yalihudhuriwa na na wawakilishi 700 kutoka Majimbo mbali mbali Barani Asia. Ilikuwa
ni nafasi kwa Kardinali Robert Sarah kuweza kujionea mwenyewe utume unaotekelezwa
na Caritas Hong kong, ambayo inendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma
na majitoleo kwa watu wenye mahangaiko mbali mbali.
Hapa pamekuwa ni mahali
pa majadiliano ya kidini na kiekumene katika mchakato wa kuwahudumia maskini na wote
wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Caritas Hong Kong imeonesha ukomavu wa hali ya
juu kwa kushirikiana taasisi mbali mbali katika kuwahudumia watu: kiroho na kimwili.
Kardinali
Sarah anasema kwamba, Caritas Hong Kong kwa sasa imeajiri wafanyakazi 5,500. Kuna
watu wa kujitolea wapatao 10, 000. Huu ni ushuhuda unaoonesha jinsi ambavyo Caritas
Hong Kong imejiingiza katika maisha na mateso ya watu, kiasi kwamba, kimekuwa ni chombo
cha huduma ya: huruma, upendo na mshikamano. Caritas kwa miaka ya hivi karibuni imeanza
kujielekeza zaidi katika majiundo makini na endelevu kwa wananchi wa Bara la Asia.
Kwa sasa Caritas imejiwekea mkakati wa kutaka kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu
cha Kikatoliki Barani Asia, kitakachochangia kwa hali na mali katika majiundo ya mtu
mzima: kiroho na kimwili na huduma ya upendo.
Mama Kanisa ameendelea kufanya
hija na Waamini wa Kanisa Katoliki nchini China kwa kutambua fursa, matatizo na changamoto
mbali mbali wanazokabiliana nazo katika kumshuhudia Kristo na Kanisa lake. Kanisa
linawatambua watoto wake na kuwakumbatia wote kwa upendo wa kimama!