2013-07-20 09:09:56

Hija ya maisha ya kiroho kwenye chemchemi ya imani, imekuwa na mafanikio makubwa!


Ndugu Cosmas Mwaisobwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei, Parokia ya Damu Takatifu ya Yesu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, ni kati ya mahujaji 41 kutoka Tanzania waliotembelea Roma, Lourdes na Nchi Takatifu, kama sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. RealAudioMP3

Anasema, hija hii imekuwa na mafanikio makubwa katika maisha yake ya kiroho, kwani kimekuwa ni kipindi cha sala, tafakari na ushuhuda. Wameonja na kushuhudia imani Katoliki kutoka kwa mahujaji mbali mbali waliokutana nao wakati wa hija yao ya maisha ya kiroho. Wamebahatika kutembelea maeneo matakatifu na yenye historia katika imani, maisha na utume wa Kanisa. Leo hii wanaufahamu mkubwa zaidi kuhusu Maandiko Matakatifu baada ya kutembelea maeneo ya kihistoria.

Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani ni changamoto kwa vijana kuhakikisha kwamba, wanaifanyia kazi pale walipo kwani ni idadi ndogo tu ya vijana ambao tayari wamekwisha ondoka kuelekea Rio de Janeiro kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, itakayowapatia nafasi ya kukutana na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuungana na Baba Mtakatifu Francisko, katika Maadhimisho ya Tukio hili la Imani.

Vijana wanakabiliwa kwa namna ya pekee na: umaskini wa hali na kipato, ukosefu wa fursa za ajira; huduma duni za elimu na afya; baadhi ya vijana wanajikuta wametumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na mmong'onyoko wa maadili.

Ndugu Cosmas Mwaisoba anawataka vijana kujiimarisha kiimani kwa kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha yao. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Familia ni chimbuko la imani, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa umakini mkubwa ili kujenga utamaduni na moyo wa kupenda kusali na kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja; Neno ambalo linamwilishwa katika matendo ya huruma. Ni vyema ikiwa kama familia itajiwekea utaratibu wa kusali pamoja!







All the contents on this site are copyrighted ©.