Baba mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amesema, atamsindikiza Papa Francisko wakati
wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana kwa Sala!
Papa Francisko, Ijumaa jioni kama sehemu ya maandalizi ya hija yake ya kichungaji
kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vija Duniani, inayoadhimishwa huko mjini
Rio de Janeiro, amemtembelea Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ili
kumwomba aweze kumsindikiza katika hija hii ya kichungaji kwa njia ya sala. Haya ni
maadhimisho yaliyokuwa yamekwishapangwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita.
Papa Francisko amemzawadia kitabu cha ratiba elekezi ya Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani, ili pale atakapoona inafaa aweze kufuatilia tukio hili
la kiimani, lakini jambo la msingi ni kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake. Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, amemhakikishia Papa Francisko kwamba,
atawasindikiza kwa sala na kwamba, amemshirikisha mang'amuzi na uzoefu wake katika
Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani huko Colony, Sydney na Madrid. Mazungumzo yao
yalitanguliwa kwa sala ya pamoja kwenye Kikanisa na baadaye, wakaendelea na mazungumzo.