2013-07-19 10:04:27

Hapa si suala la malumbano ya kisiasa na kidini, bali ni mambo yanayogusa utu na heshima ya binadamu!


Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanakabiliwa na changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Maisha ni kati ya tunu msingi ambazo watu wengi waliziheshimu na kuzithamini, lakini katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, uhai wa binadamu si mali kitu!

Lakini, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha kwani unapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, kuna uhusiano wa pekee kwani mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, jambo linaloonesha uhusiano wa pekee kati ya Mungu na binadamu. Kumbe, hili si suala la mapambano kati ya wanaharakati na Kanisa au wanasiasa na Kanisa, bali ni mada inayogusa utu na heshima ya binadamu kwani sera za utoaji mimba ni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Uhai ni haki ya kila binadamu na kwamba, haki hii haiwezi kutengeliwa na wanaharakati au wanasiasa.

Mama Kanisa anadhamana na wajibu wa kusimama kidete kutetea Injili ya Uhai kwani ni sauti ya wanyonge na kwamba, kila mtu anayo dhamana na wajibu wa: kuheshimu, kulinda, kupenda na kuhudumia Injili ya Uhai; kwa kukataa katu katu kukumbatia Utamaduni wa kifo. Kuna maendeleo makubwa ya sayansi na huduma ya dawa; mambo yanayopania kulinda na kuboresha afya ya binadamu, lakini inasikitisha kuona kwamba, hata katika maendeleo haya Utamaduni wa kifo unaendelea kushika kasi ya ajabu, kiasi kwamba, Uhai wa binadamu umekuwa ni kama kichokoo ambacho watu wanaweza kukichezea kama wanavyopenda.

Hii ni sehemu ya tafakari ya kina kutoka kwa Askofu mkuu Michael Neary katika Maadhimisho ya Siku ya Injili ya Uhai, iliyofanyika hivi karibuni Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland. Ni wajibu na dhamana ya Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya Utamaduni wa Kifo, kwani huu ni wajibu msingi wa kimaadili kama ilivyo pia kwa dini kubwa duniani.

Injili ya Uhai inawagusa wote; mama na mtoto ambaye bado yuko tumboni mwake, kwani tumbo la mama ni nyumba ya kwanza ya binadamu. Ni mahali ambapo mtoto anaanza kuonja upendo na furaha kutoka kwa wazazi wake. Ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu hatari inayoweza kuwepo kati ya maisha ya mama na mtoto! Lengo kuu daima liwe ni kwa ajili ya kuokoa maisha ya binadamu na wala si kutaka kuyaangamiza kwa makusudi kutokana na ubinafsi. Hakuna sheria ya utoaji mimba inayolenga kuokoa maisha ya binadamu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linabainisha kwamba, sheria ya utoaji mimba nchini humo ni jambo ambalo haliwezi kukubalika kimaadili. Kanisa bado linaendelea kushikamana na kuwaonjesha huruma wale ambao wanasikitika mara baada ya kushiriki katika tendo la utoaji mimba; linajitaidi kuwaelewa wale ambao wanakabiliwa na maamuzi machungu kuhusu suala zima la utoaji mimba pamoja na kuwasaidia wale wote wanaoamua kuenzi Injili ya Uhai.

Maaskofu Katoliki kutoka Ireland wanasema wanasukumwa na msimamo wao wa kiimani kuthibitisha kwamba, kila haki msingi ya binadamu, ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku za usoni inatokana na uelewa kwamba maisha ni kito cha thamani, ni matakatifu na ni zawadi kutoka kwa Mungu; changamoto kwa kila mtu kukumbatia Injili ya Uhai.








All the contents on this site are copyrighted ©.