2013-07-19 10:40:54

Afya ya akili Barani Afrika, haijapewa kipaumbele cha kutosha!


Wagonjwa wenye matatizo ya afya ya akili Barani Afrika wanaendelea kutumbukia katika balaa la umaskini na wengi wao hawapati huduma makini, ambayo ingeweza kuwasaidia kupona kutokana na maradhi yanayowasumbua. Hali hii inachangiwa pia na uhaba mkubwa wa wataalam wa afya ya akili, ukosefu wa miundo mbinu na vifaa na kwamba, wagonjwa ambao wanahitaji tiba hawaipati.

Hii ni changamoto inayotolewa na Wataalam wa afya ya akili wanaoendelea na mkutano wao mjini Kampala, Uganda, unaopania pamoja na mambo mengine, kuwajengea watu uwezo wa afya ya akili Barani Afrika. Kenya ambayo ina watu millioni 44 inahudumiwa na watalaam 83 na kwamba, nchi nzima ina hospitali moja tu inayowahudumia wagonjwa wa akili. Kuna jumla ya watu millioni 3.6 ya Wakenya wenye matatizo ya afya ya akili, watu ambao wamekataliwa na familia zao na wanaishi katika hali mbaya sana!

Wataalam wa afya ya akili kutoka Barani Afrika wanazihamasisha Serikali zao kuwekeza zaidi katika afya ya akili; kwa kuwaandaa wataalam watakaotoa huduma makini kwa wagonjwa wa afya ya akili, huku wakionesha moyo wa huruma na mapendo. Wagonjwa wa afya ya akili wanahusishwa na imani za kishirikina na mara nyingi hawapewei msaada unaotakiwa. Huduma ya afya, imekuwa ikitolewa kwa watu wachache "wenye vijisenti vyao".

Uganda ambayo ina watu millioni 33 na ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, ina jumla ya watalaam 33, hii ina maana kwamba, kila mtaalam anahudumia wastani wa watu millioni moja!







All the contents on this site are copyrighted ©.