2013-07-18 07:52:35

Vijana msitafute uhuru usiokuwa na mipaka!


Mheshimiwa Padre Pascual Chaves Villanueva, Mkuu wa Shirika ya Wasalesiani wa Don Bosco katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika vijana kuhakikisha kwamba, wanamwilisha kwa ukamilifu ule ubinadamu wa Yesu katika maisha yao, kwa kutolea ushuhuda makini tunu msingi za Kiinjili.
Kanisa linaendelea kujikita katika changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Uinjilishaji Mpya, ili kuwawezesha waamini kugundua tena ndani mwao ile furaha ya imani katika Mwenyezi Mungu, kwani kwa sasa kuna vugu vugu kubwa la ukanimungu, linalopania kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vya binadamu; kwa maneno mengine, mwanadamu anatafuta uhuru usiokuwa na mipaka!
Kuinjilisha maana yake ni kuweka chachu ya tunu msingi za Kiinjili katika maisha ya watu ili hatimaye, waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu pamoja na kutambua Mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Uinjilishaji mpya unalenga kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha na vipaumbele vya nwanadamu.
Ili kufanikisha azma hii, kwanza kabisa Mwinjilishaji hana budi kuhakikisha kwamba, ana upendo wa dhati kwa Mwenyezi Mungu; upendo anaoendelea kuuboresha kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Ni mtu ambaye kimsingi, moyo wake hauelemewi na takataka za dunia hii. Ni changamoto ya mtu mwenyewe kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha yake; akijiweka wazi na mkweli mbele ya Mwenyezi Mungu anayeufahamu undani wa maisha yake.
Padre Chaves Villanueva anasema, kwa bahati mbaya, vijana wengi wanaishi katika ombwe na hali ya kufikirika na baadhi yao wameshindwa kutumia vyema moyo na akili zao zao, wamebaki kufuata mkumbo wa makundi ya vijana wanaowazunguka. Kwa maneno mengine, vijana wengi, utulivu ni zero! Kutokana na mwelekeo huu inakuwa ni vigumu kabisa kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu! Mwanadamu anakabiliana na madonda makubwa katika moyo wake, yanayohitaji kwanza kabisa: kusikilizwa, kueleweka pamoja na kuponywa.
Ulimwengu unawahitaji Mitume wa Yesu watakaojitoa kimaso maso kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini: ile furaha, wasi wasi na mashaka ya kutaka kukutana na Kristo; mashaka ambayo wakati mwingine, yamejificha kutoka katika undani wa maisha ya kijana mwenyewe, ili kuweza kushirikishana uelewa wa kina kuhusu Mwenyezi Mungu. Vijana wanapaswa kukumbuka kwamba, ni Yesu Kristo peke yake anayeweza kuwaponya majeraha ya mioyo yao.
Ili kupata uponyaji wa ndani, kuna haja kwa vijana wenyewe kupiga hatua mbele kwa kumtambua, kujenga na kuimarisha uhusiano na Yesu; wampende na hatimaye, waweze kumfuasa kwa moyo wote. Hii ni hija inayofanyika katika Jumuiya ya Waamini. Ukombozi wa mwanadamu umeletwa na Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu na anaendelea kufanya hija na Wafuasi wake ndani ya Kanisa.
Ni kwa njia ya Kanisa, vijana wanaweza kukutana na Jumuiya inayomwamini Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, aliyezaliwa bila kuumbwa, Mwenye Umungu mmoja sawa na Baba; Aliyeteswa, Akafa na Kufufuka kutoka katika Wafu. Inawezekana kwamba, vijana wakakumbana na vizingiti vikubwa katika safari ya maisha yao ndani ya Kanisa; hii ni sura ya ubinadamu inayooneshwa na Kanisa, kwani itakumbukwa kwamba, Kanisa lina asili mbili; ile ya Kimungu kwani limeanzishwa na Kristo mwenyewe na ile ya kibinadamu kwani amelikabidhi kwa binadamu wenye karama na mapungufu yao, lakini watu ambao wako katika mchakato wa kujitakatifuza zaidi na zaidi.
Kanisa ni Mama wa waamini wote anayependa kumkumbatia kila mtoto kwa upendo wa kimama, ili kumwezesha kupata utambulisho na fursa ya kuweza kukutana na Kristo kwa njia ya: Sala, Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma. Ni mwaliko kwa vijana kujishikamanisha na Kanisa, kwani kamwe halizeeki na ujana wake ni wa milele. Huu ni mwaliko kwa vijana kujifunza namna yak usali na kutafakari; tafakari inayogeuzwa kuwa ni sala pamoja na kuendelea kuwa wazi kwa Mapaji na Karama za Roho Mtakatifu, anayetaka kuwakirimia mapaji haya ili waweze kuishi ubinadamu wao katika utimilifu wake.
Wainjilishaji na Walezi katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo; vijana wa kizazi kipya wanapenda kusikia Neno la Mungu likitangazwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha; Neno linalofanyiwa tafakari ya kina katika sala, ili kukuza na kuimarisha Imani. Mama Kanisa anawapenda vijana kwa moyo wa Kristo mchungaji mwema, aliyethubutu kuyamimina maisha yake kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Imani haina budi kuwa na ule uwezo wa kusikiliza kilio cha: maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; Imani inayomwilishwa kwa njia ya Matendo ya Huruma yanayomwonesha Mungu kuwa ni Upendo.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2013 unaongozwa na kauli mbiu “Nasi tumelifahamu pendo alilonalo Mungu, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake.”. Ujumbe huu uwasaidie vijana kutafakari fadhila ya upendo pamoja na kujitahidi kuimwilisha katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vyao.
Imekwishagota takribani miaka 200 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Bosco, hali za kijamii, kisiasa na kiuchumi zimebadilika sana, kumbe, kuna haja ya kusoma alama za nyakati kwa kukazia na kuwekeza katika sekta ya elimu itakayosaidia katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani; kwa kujiondoa kutoka katika sera, falsafa na siasa zinazomdumaza kijana na kuanza hija ya maisha ya kiutu na ukomavu wa Kikristo. Vijana wanapaswa kuelimishwa ili waweze kuwajibika barabara katika maisha na vipaumbele vyao kwa sasa na kwa siku za usoni!
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, ni matumaini ya Kanisa kwamba, walau vijana wataweza kuonesha uso wa tabasamu la nguvu, kwa kuguswa na Habari Njema ya Wokovu; kwa kupenda na kupendwa ili kuvuka vizingiti katika hija ya maisha ya vijana, vinavyowafanya wakati mwingine kushindwa kuelewana miongoni mwao na hatimaye, kulichukia Kanisa.
Padre Pascual Chavez Villanueva anahitimisha ujumbe wake kwa vijana kwa kusema kwamba, Kijana mwenye imani thabiti ni mmissionari hodari wa yesu, anapaswa kuonesha ile furaha iliyomo ndani mwake; kwa kupenda na kupendwa; ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni watangazaji mahiri wa Habari Njema ya Wokovu katika Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo.
Vijana watangaze Injili ya Kristo kwa: Imani, Upendo na Matumaini; daima wakijitahidi kuwa ni mashahidi wenye ari, nguvu na kasi mpya, wakishijishikamanisha na Yesu Kristo Mkombozi wa Ulimwengu. Anawatakia kila la kheri na baraka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, sanjari na Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, itakayofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.