Siku ya Vijana Duniani: Maadhimisho ya Njia ya Msalaba
Njia ya Msalaba kwenye ufuko wa Bahari wa Copacabana, eneo lililopambwa kwa misitu
ya asili na maji, mambo yanayodhihirisha sifa na utukufu wa kazi ya Uumbaji ambayo
Mwezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kuitunza na kuiendeleza, patakuwa ni mahali pa tafakari
ya kina kuhusu Fumbo la Msalaba, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani
huko Rio de Janeiro.
Ibada hii
ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia,
itashuhudia pia uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye kwa mara ya kwanza atakuwa
anashiriki Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Lakini itakumbukwa kwamba, Jumapili
ya Matawi, alisherehekea Siku ya Vijana Kijimbo na kuwaalika vijana kumuunga mkono
wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani mjini Rio de Janeiro. Ibada hii inatarajiwa
kuchukua takribani muda wa saa moja na nusu na itafanyika katika mandhari ya kuvutia
na kutafakarisha.
Nafasi ya Yesu wakati wa Njia ya Msalaba itafanywa na vijana
mbali mbali na kwamba, itakuwa ni nafasi ya vijana kutolea ushuhuda wa imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake. Taarifa inabainisha kwamba, kutakuwa na vijana thelathini watakaolinda
Msalaba wakati wa Njia ya Msalaba. Msalaba wa Siku ya Vijana Duniani umeanza kutembezwa
nchini Brazil na nchi jirani kuanzia mwaka 2011 mara tu baada ya Maadhimisho ya Siku
ya Vijana Duniani yaliyofanyika mjini Madrid, Hispani na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu
Mstaafu Benedikto wa kumi na sita.
Hili ni tukio ambalo bado linakumbukwa
na vijana wengi, hasa usiku ule Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita alipoamua
kubaki na vijana wakati mvua kubwa ilipokuwa inanyeesha, akaonesha moyo na upendo
wa kibaba na kichungaji. Kuna vijana mia mbili kutoka katika nchi mbali mbali watabeba
bendera wakati wa Maadhimisho ya Njia ya Msalaba.
Mambo yanaendelea kupamba
moto nchini Brazil, tayari kumpokea na kumkirimia Baba Mtakatifu Francisko wakati
wa hija yake ya kwanza ya kichungaji nje ya Italia.