2013-07-18 07:42:19

Maadhimisho ya Siku ya Vijana, Yaani we acha tu!


Vijana kumi na wanane kutoka Sudan wanatarajiwa kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro. Kila Jimbo limebahatika kutoa vijana wawili kuwa ni wawakilishi katika Maadhimisho ambayo huwakusanya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kundi hili litaongozwa na Padre Philip Bingo kutoka Idara ya Utume wa Vijana kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan. RealAudioMP3

Hapa ikumbukwe kwamba, licha ya kura ya maoni iliyopelekea Sudan ya Kusini kuwa ni nchi huru inayojitegemea, lakini Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan bado ni moja. Vijana hawa wameanza maandalizi ya kuangalia kile ambacho wanaweza kuchangia katika hija hii ya maisha ya imani na kwa namna ya pekee, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani.

Shirika la Kipapa kwa ajili ya Makanisa hitaji limegharimia safari ya vijana kutoka Sudan. Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 ni ”Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi”. Maadhimisho haya ni kipindi cha sala, tafakari, katekesi ya kina na burudani. Vijana watapata pia fursa ya kuweza kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo kama sehemu ya ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Taarifa zinaonesha kwamba, zaidi ya vijana 84, 000 wamejiandisha kwa ajili yakujitolea kutoa huduma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka huu. Zaidi ya ndege 149 zimekwishathibitisha kupeleka mahujaji wakati wa Maadhimisho haya. Wachunguzi wa mambo ya maisha na utume wa vijana wanasema, ”kwa hakika mwaka huu, Rio hapatoshi” hasa ikizingatia kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa ana mvuto mkubwa kwa watu atashiriki kwa namna ya pekee kabisa!.








All the contents on this site are copyrighted ©.