2013-07-17 09:44:34

Watu wamekata tamaa kutokana na ukosefu wa misingi ya haki, amani na utulivu!


Waamini na wananchi wenye mapenzi mema kutoka Jamhuri ya Wananchi wa Afrika ya Kati, tarehe 21 Julai 2013 wataungana kusali kwa ajili ya kuombea amani na haki jamii nchini humo. Waamini wanatambua kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha pia mwanadamu, kumbe, kusali kwa ajili ya kuombea amani ni sehemu ya wajibu huu na sanjari na wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana ya kulinda na kudumisha amani na utulivu.

Wamissionari wa Shirika la Wakarmeli wanaotekeleza utume wao huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, wameamua kumlilia Mwenyezi Mungu ili aweze kusikiliza sauti ya kilio chao kutokana na taabu na mahangaiko ya wananchi wengi wanaoteseka kutokana na athari za vita na misigano ya kijamii. Wamissionari hawa wanataka kuombea amani na utulivu.

Makanisa mengi yamenajisiwa, Parokia zimeporwa; vituo vya huduma ya afya na shule zimeharibiwa kiasi kwamba, watu wengi wamekata tamaa ya maisha. Waamini wanatambua kwamba, nguvu ya upendo na sala inaweza kuleta mabadiliko katika mioyo ya watu sanjari na kuanza mchakato wa kujenga na kudumisha haki, msamaha na upatanisho wa kweli kama njia ya kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Nguvu ya Injili ninyenzo ya kweli ya maendeleo ya mwanadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.