SECAM, hatuwezi kukaa kimya wakati wananchi wa Bara la Afrika wanaendelea kuteseka,
kunyanyasika na kudhulumiwa!
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, limehitimisha
mkutano wake wa kumi na sita, uliofunguliwa hapo tarehe 9 hadi 14 Julai 2013 kwa kuwataka
viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua zitakazosaidia maboresho ya maisha
ya wananchi wa Bara la Afrika, badala ya mwelekeo wa sasa ambao umelifanya Bara la
Afrika kuwa kama "kichwa cha mwenda wazimu" kila mtu akifika anataka kupora raslimali
na utajiri wa Bara la Afrika kwa ajili ya mafao binafsi.
Mkutano mkuu wa SECAM
umeongozwa na kauli mbiu "Kanisa kama Familia ya Mungu Barani Afrika katika huduma
ya upatanisho, haki na amani". Mkutano umebainisha dira na mwelekeo wa utekelezaji
wa Maazimio ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika pamoja na Waraka wa Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, Dhamana ya Afrika.
Maaskofu wa
SECAM wanawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema Barani Afrika, kuhakikisha kwamba,
wanasimama kidete kulinda na kutetea haki jamii, usawa, utu na heshima ya binadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Wajumbe
wamezitaka Serikali Barani Afrika kusitisha vita inayoendelea kuleta maafa makubwa
sanjari na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu. Wanasema, umefika wakati wa kuweka
mikakati itakayosaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa upatanisho, haki na amani
kwa ajili ya mafao ya wengi.
Katika mateso na mahangaiko ya watu wengi Barani
Afrika, Maaskofu wa SECAM wanasema, kamwe hawataweza kukaa kimya, kwani vita na mahangaiko
ya watu wengi wa Afrika inaonekana kusahaulika machoni pa Jumuiya ya Kimataifa. SECAM
inawaomba viongozi wa kimataifa kuyavalia njuga matatizo ya Bara la Afrika ili kupata
ufumbuzi wa kudumu.
Wajumbe wa SECAM wamesikitishwa na vita na kinzani za kijamii
zinazoendelea kujitokeza huko: Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nchi zilizoko kwenye Pembe
ya Afrika, Mali, Nigeria, Sudan ya Kusini, Madagascar, Rwanda, Uganda, Tunisia na
Misri.