2013-07-16 07:46:17

Chimbuko na maana ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013


Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alifurahia sana kuwa kati ya vijana, kiasi kwamba, akapiga moyo konde na kuanzisha siku ya Vijana Duniani kunako mwaka 1985. RealAudioMP3

Akahimiza siku ya vijana kijimbo, inayoadhimishwa kila mwaka Jumapili ya Matawi, ili kutoa nafasi kwa Maaskofu mahalia kukutana na kufahamiana na vijana katika Majimbo yao. Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili alitambua kwamba, vijana ni jeuri na nguzo ya Kanisa kwa sasa na kwa siku za usoni, ni watu waliokuwa wanahitaji kupea majiundo makini ili waweze kutekeleza dhamana na majukumu katika maisha yao ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Papa Yohane Paulo wa pili aliwahimiza Maaskofu na walezi wa vijana kuhakikisha kwamba, wanawajengea vijana maana ya maisha, hasa kutokana na ukweli kwamba, vijana katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia wanakumbana na changamoto mbali mbali, kiasi hata cha kuwafanya wapoteze dira na mwelekeo wa maisha: kiroho na kiutu!

Dunia ya leo inaendelea kucharuka kwa maendeleo, lakini kwa bahati mbaya, maendeleo haya yanamjengea mwanadamu upweke hasi, unaoweza kusababisha kutema zawadi ya maisha, hali inayojionesha kwa vijana wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili kwa kuanzisha Siku ya Vijana Duniani, alitamani kuona kwamba, Kanisa linajitwika dhamana ya kuwajengea vijana: imani, matumaini na mapendo, vijana ambao watakuwa ni wadau wakuu wa Uinjilishaji miongoni mwa vijana wao katika ulimwengu wa utandawazi unaosheheni kila dalili za ukanimungu!

Hii ni tafakari ya kina kutoka kwa Padre Thomas Rosica, Muasisi wa Taasisi ya Kikatoliki ya Mawasiliano ya Jamii nchini Canada na Mratibu mkuu wa Siku ya Vijana Duniani kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Canada. Anasema, vijana wanapaswa kuwa ni nyenzo za Uinjilishaji wa Kimaadili.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanajikita kwa namna ya pekee katika Ibada, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Katekesi makini na endelevu; Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Upatanisho inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.

Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, vijana wanapata nafasi ya kushiriki katika Njia ya Msalaba, kuwakumbusha kwa mara nyingine tena, Fumbo la Msalaba, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vijana wanapata kusikiliza kwa mara nyingine historia ya watu waliojitoa kimaso maso kwa ajili ya Mungu na jirani, katika huduma na ushuhuda amini, hata wakadiriki kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Hawa ndio watakatifu na waungama dini, wanaoendelea kujitokeza kila siku ya maisha, kama Baba Mtakatifu Francisko anavyokazia.

Siku ya Vijana Duniani, ni kipindi cha kufanya hija ambayo kimsingi ni safari kutoka katika undani wa maisha yao, kutoka katika maeneo yao, lakini zaidi kutoka katika utupu wa maisha, ili kuanza mchakato wa kukutana na Yesu, chemchemi ya furaha na maisha ya uzima wa milele. Hizi ni siku za huduma kwani kuna umati mkubwa sana wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaohudumiana na kushirikishana tone la upendo.

Siku za Vijana Duniani, zimekuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, hapa wengi wamepata kuonana na kufahamiana kiasi kwamba, wakaanzisha uchumba na hatimaye, wakafunga pingu za maisha. Kuna vijana na wasichana wengi ambao wameguswa kwa namna ya pekee, leo hii ni Mapadre na Watawa. Mambo haya msingi ni muhimu sana katika maisha na utume wa vijana ndani ya Kanisa. Kilele cha Maadhimisho haya kinawajengea vijana moyo wa Ibada na uchaji wa Mungu. Njia ya Msalaba na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni kati ya matukio makuu yanayohitimishwa kwa Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, kama kielele cha maisha na utume wa Kanisa.

Padre Thomas Rosica anasema kwamba, vijana wa kizazi kipya wanahitaji kuona mifano ya watu watakatifu, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, Mama Theresa wa Calcutta ni kati ya mifano hii hai na muhimu sana ndani ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, katika uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alibahatika kuwatangaza wenyeheri 482 kuwa Watakatifu na Watumishi wa Mungu 1, 338 kuwa Wenyeheri. Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2011, iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Madrid, Hispania, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, alikuwa ni kati ya Watakatifu wasimamizi wa siku hii, Jambo la kupendeza na kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Watu wengi wamevutwa na kuguswa katika maisha na utume wao kwa mfano wa utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, aliyewachangamotisha vijana kutoogopa kumfungulia Kristo malango ya mioyo na maisha yao, kwani hakuna kitu wanachoweza kupoteza wakimkubali Kristo kuwa ni Bwana na Mwalimu wa maisha yao, zaidi wataendelea kufaidika na kupeta katika maisha! Watu wengi wameguswa na maisha na mfano wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kiasi kwamba, wamekuwa kweli ni watu wapya!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yanaendeleza historian a mang’amuzi kwamba, hili ni tukio la Kikanisa! Ni tukio ambalo limeshuhudiwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kama muasisi wake, likaendelezwa na kuboreshwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, na wachunguzi wa mambo wanasema, Mwaka huu, Papa Francisko anatarajiwa kufunika! Haya ni maadhimisho ya vijana kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama njia ya kurithisha imani, matumain, mapendo, vipaumbele na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana.

Ikumbukwe kwamba, maisha ya Kikristo ni hija endelevu ya watu wa Mungu pamoja na Kristo mwenyewe kama alivyofanya kwa Wafuasi wake wa Emmaus. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani anasema Padre Thomas Rosica si kipindi cha muujiza unaolenga kutatua matatizo na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa vijana, utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, bali hapa ni mahali ambapo Vijana kwa kushirikiana na Kanisa, wanataka kujenga matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ni hija inayojionesha katika uhalisia wa maisha ya kila siku, changamoto endelevu iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita! Kanisa linapenda kutangaza ujana wake kwa kushikamana na vijana, kwani kwa njia hii haliwezi kuzeeka! Vijana wanaendelea kuwa ni mashahidi ya furaha iliyooneshwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Mama Kanisa kwa namna ya pekee, anawahamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika mchakato unaopania kuwaonjesha furaha, matumaini, imani na umoja. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwahi kusema, Kanisa ni hai na kamwe haliwezi kuzeeka wala kuota mvi! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni ushuhuda wa ukweli huu!

Imehaririwa na
Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.