Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mkutano
wake wa kumi na sita, uliokuwa unafanyika mjini Kinshasa, DRC, imekuwa ni fursa kwa
wajumbe wa SECAM kupembea kwa kina na mapana, Kanisa kama Familia ya Mungu inayokiri
na kuungama: Ubatizo na imani moja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na Neno la Mungu,
inavyowajibika katika kutunza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho Barani
Afrika.
Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum
na Radio Vatican mjini Kinshasa, DRC anasema kwamba, Bara la Afrika kwa sasa linawaka
moto kutokana na kinzani za vita, migogoro ya kijamii, kitamaduni, kisiasa na kidini;
kuna ukosefu mkubwa wa haki msingi za binadamu; rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika
unaendelea kupokwa na wajanja wachache; rushwa na ufisadi ni mambo ambayo kwa sasa
yamekuwa ni wimbo usiokuwa na mchezaji!
Kanisa Barani Afrika limebainisha mbinu
mkakati utakaoliwezesha kuwa kweli ni chombo cha haki, amani na upatanisho, kama sehemu
ya utekelezaji wa mikakati ya kichungaji iliyobainishwa na Mababa wa Awamu ya Pili
ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika na hatimaye, hati baada ya Sinodi hii ikatolewa na
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Haki, amani na upatanisho ni tunu
muhimu sana katika maisha ya mwanadamu katika ngazi mbali mbali.
Askofu Ngalalekumtwa
anasema, kila mtu anachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa ni chombo cha haki, amani
na upatanisho Barani Afrika. Amani inapaswa kupata chimbuko lake katika undani wa
moyo wa mwanadamu. SECAM imepitisha maazimio katika utekelezaji wa Waraka wa Dhamana
ya Afrika, Africae Munus iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita. Waraka huu si mapambano ya meza wala makabati, bali unapaswa kutekelezwa ili
dunia iwe na amani na Bara la Afrika liweze kutoa mchango wake katika kurejesha misingi
ya haki, amani na upatanisho.