2013-07-13 09:14:46

Mfungo wa Ramadhani kiwe ni kipindi cha kujenga na kudumisha haki, amani na utulivu!


Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kipindi cha swala, kufunga na kutoa sadaka. Ni wakati ambapo mwamini wa dini ya Kiislam anahimizwa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu huku akionesha upendo kwa jirani yake. Ni ujumbe kutoka kwa Patriaki Fouad Twal, wa Yerusalemu, wakati huu ambapo Waamini wa dini ya Kiislam wanaendelea na Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Anapenda kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na waamini wa dini ya Kiislam, akiwaalika kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia moyo wa upendo na mshikamano, kwa ajili ya kuwasaidia wale wanaoteseka na kwa namna ya pekee watoto, wanawake na wazee nchini Syria.

Waamini wa dini mbali mbali wajifunze kujenga na kuimarisha utamaduni wa upendo kwa kuepuka kabisa chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi na vitendo vyote vinavyopelekea ukosefu wa misingi ya haki na amani. Inasikitisha kuona kwamba, waamini wengi wa dini ya Kiislam wanaadgimisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakati ambapo kuna vita na kinzani zinaendelea kufuka moshi sehemu mbali mbali za dunia.

Patriaki Twal anaungana na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon kuwataka wadau mbali mbali kujibidisha kutunza amani na utulivu wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Anawatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema huko Mashariki ya Kati, wanaoishi katika vurugu na kinzani, kutafuta suluhu ya kinzani hizi kwa njia ya amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.