Kuna uhusiano wa pekee kati ya: shule, familia na parokia
Kanisa Katoliki Barani Afrika limekuwa ni mdau mkubwa katika utoaji wa huduma kwenye
sekta ya elimu kuanzia kwenye ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu. Katika mchakato
wa Uinjilishaji wa kina, Kanisa nchini Mauritius linapenda kujikita katika sehemu
kuu tatu yaani: Familia, Shule na Parokia. Huu ni mkakati wa Uinjilishaji wa kina
unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2016.
Mwaka
wa kwanza, Kanisa litajikita zaidi kwa kukazia majiundo makini shuleni, kwa kuwekeza
zaidi na zaidi, ili elimu inayotolewa na Kanisa Katoliki nchini humo iendelee kukidhi
viwango na mahitaji ya wananchi wa Mauritius; kwa kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuihudumia
nchi yao kwa moyo na ari kubwa zaidi. Ustawi na maendeleo ya nchi yanapata chimbuko
lake katika msingi bora wa elimu. Kanisa Katoliki nchini Mauritius linatambua na kuthamini
mchango unaotolewa na Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika sekta ya elimu.
Shule na taasisi za elimu zinapaswa kuwa ni madaraja yanayojenga na kuimarisha
umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua na kuthamini tofauti za kidini, kiimani
na kitamaduni, lakini mambo yote haya yawe ni sehemu ya utajiri wa wananchi wa Mauritius
na kamwe yasiwe ni kizingiti wa kikwazo cha kuwagawa watu. Maadili na utu wema na
mambo msingi katika sekta ya elimu, vinginevyo vijana wanaweza kujikuta wanaelemewa
mno na malimwengu kiasi cha kushindwa kutambua na kuenzi tunu msingi za maisha na
maadili ya Kiafrika kutokana na athari za utandawazi.
Hii ndiyo mikakati
ya shughuli za kichungaji iliyopembuliwa hivi karibuni na Askofu Maurice Piat wa Jimbo
la Port-Louis, nchini Mauritius. Kanisa linapenda kuangalia kwa namna ya pekee dhamana
na utume wake katika sekta ya elimu, kwa kukazia utofauti unaojisimika katika umoja
na mshikamano, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya: Elimu, Parokia na Familia kama
inavyobainishwa kwenye "Mradi wa Kleopas".
Kanisa linapenda kujikita zaidi
pia katika kuimarisha Katekesi, ili waamini waweze kufahamu kuhusu Mafundisho tanzu
ya Kanisa na wawe tayari kuyatolea ushuhuda katika maisha na vipaumbele vyao. Jamii
ijifunze kujenga na kuimarisha majadiliano ya kidini na kiimani, yanayofumbatwa katika
msingi wa ukweli na uwazi pamoja na kuthaminiana. Waamini katika mchakato kama huu,
watambue Imani ya Kanisa Katoliki pamoja na kuendelea kuwanoa Makatekista, ili waweze
kutekeleza utume wao kikamilifu katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi ya ajabu.
Vyama
vya kitume na familia katika Parokia ni muhimu sana katika kujenga na kuimarisha utambulisho
na mshikamano wa Familia ya Mungu inayowajibika. Waamini washirikishe karama, vipaji
na taaluma zao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika ngazi mbali
mbali za maisha na utume wa Kanisa. Kila mwamini anakumbushwa kutekeleza dhamana
na wajibu wake kama Mbatizwa na raia mwema.