Cheche za Mwanga wa matumaini kutoka kwa Mwenyeheri Yohane Paulo II
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni cheche ya mwanga wa matumaini na zawadi kubwa
ambayo Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili ameliachia Kanisa na kwamba, matunda ya Maadhimisho
haya ni juhudi za mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mabaraza ya
Maaskofu katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kabla, wakati na baada ya Maadhimisho
haya!
Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yana umuhimu wa pekee kwani, kunako mwaka
1987, kwa mara ya kwanza Siku ya Vijana Duniani iliadhimishwa huko Buenos Aires, nchini
Argentina. Hapa watu wakashuhudia vijana wakiungana na Baba Mtakatifu Yohane Paulo
wa pili, aliyewaambia vijana kwamba, yuko kati yao, ili kuwasikiliza, kuzungumza na
kusali pamoja nao! Vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa, changamoto kwa vijana kuwa
ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana wanahamasishwa kuwa makini dhidi ya
wote wanaotaka kufisha matumaini yanayobubujika kutoka katika undani wa mioyo yao!
Hii
ni tafakari ya kina inayotolewa na Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa
kwa ajili ya Walei. Anasema, Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani yaliandaliwa
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na sasa itaadhimishwa na Papa
Francisko, Myesuiti wa kwanza kuchanguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro na na
Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini.
Baba Mtakatifu Francisko anawaambia
vijana kwamba, anaungana na watangulizi wake, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili na Baba
Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Maadhimisho haya, kwa imani na
matumaini makubwa. Ili kufanikisha Maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko alikuwa
amewaalika vijana kujiandaa kikamilifu kiroho, kwa kutambua kuwa hili ni tukio la
kiimani na hija ya maisha ya kiroho. Ni mwaliko kwa vijana kutoka katika undani na
utupu wa maisha yao ya vijana ili kuwaendele wengine wanaoishi na kusukumizwa pembezoni
mwa Jamii kwani njia za Bwana zina maajabu mengi.
Maadhimisho ya Mwaka 2013
huko Rio de Janeiro, Brazil yanaongozwa na kauli mbiu ”Basi enendeni, mkawafanye mataifa
yote kuwa wanafunzi”. Huu ni mwaliko anasema Kardinali Rylko kwa vijana kukuza na
kudumisha moyo wa kimissionari ndani mwao, huku wakiendelea kuchangamotishwa na ujumbe
wa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Uinjilishaji Mpya kwamba, mchakato wa
Uinjilishaji mpya unapania kutangaza Imani ya Kikristo.
Vijana wanaotoka Amerika
ya Kusini wanahamasishwa pia kuwani Wamissionari katika nchi zao, kwani vijana wana
kiu ya kutaka kusikiliza Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa miongoni mwao kwa njia
ya ushuhuda wa maisha na imani tendaji. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, utume na
maisha ya Kanisa yako mikononi mwa vijana wenyewe! Ni dhamana ya Mama Kanisa kuhakikisha
kuwa inaibua mbinu mkakati utakaofanikisha kuasha dhamiri nyofu, ari na moyo wa kimissionari;
miito na huduma ndani ya Kanisa mintarafu mwongozo na Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 yanakwenda sanjari na
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, mwaliko na changamoto kwa vijana kutambua mafundisho
tanzu ya Kanisa; kukiri imani kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya uhsuuda wa maisha
adili; Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Sala. Vijana wajitaabishe kuifahamu
Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki; muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Amri
za Mungu na Maisha ya Sala.
Hii ni amana ya Kanisa iliyohifadhiwa kwa zaidi
ya miaka elfu mbili iliyopita. Vijana wanaalika kujisomea na kutafakari Katekesimu
Mpya ya Kanisa Katoliki kwa moyo mkuu na endelevu. Kanisa Katoliki nchini Brazil linawasubiri
vijana kwa moyo wa upendo na ukarimu
Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani
si haba! Kanisa linaweza kufanya tathmini ya kina ili kuangalia ni matunda yepi ambayo
yamekwishajitokeza katika kipindi chote hizi na wapi ambapo Kanisa linapaswa kuboresha
ili kufanikisha Maadhimisho haya. Vijana wanapaswa kugundua kwamba, Yesu ni njia,
ukweli na uzima; Kanisa kwa upande wake ni Mama, Mwalimu na Rafiki wa kweli. Khalifa
wa Mtakatifu Petro ni kiongozi ni mwenza wa hija ya maisha ya kiroho na kiutu; ni
rafiki ambaye vijana wanaweza kumtumainia. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni
maabara au karakana za imani, kama alivyopenda kusema, Mwenyeheri Yohane Paulo wa
pili, enzi zake!
Hapa pamekuwa ni chemchemi na chimbuko la miito mbali mbali
ndani ya Kanisa na kwamba, Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo,
limejikuta likiwa na sura ya ujana, pasi na makunyanzi; Kanisa ambalo limewasukuma
vijana kuendelea kujiamisha kwa Kristo na Kanisa lake. Vijana kwa nyakati hizi wamekuwa
kweli wadau wa heri za Mlimani, Manabii wa nyakati hizi na vyombo vya upendo wa Mungu
kwa binadamu.
Vijana watambue kwamba, Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani
ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa lake; mahali ambapo vijana wanaweza kuchota tunu msingi
za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni; ni chombo muhimu sana cha Unjilishaji Mpya;
mahali ambapo wenye kiu na njaa ya maisha ya uzima wa milele wanaweza kushibishwa!
Hili ni Jukwaa la majadiliano kati ya Kanisa na Vijana, changamoto kwa pande
hizi mbili anasema Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kusikilizana kwa makini. Hiin
i epifania na ufunuo wa imani; ni mahali pa kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli
za kichungaji kwa ajili ya vijana. Hii ni amana na urithi mkubwa kutoka kwa Papa Yohane
Paulo wa Pili kwa ajili ya Kanisa.
Maadhimisho ya Mwaka huu anasema Kardinali
Stanislaw Rylko ni njia ya kuona dhamana ya Uinjilishaji Mpya na fahari ya kuwa Mkristo.
Wachunguzi wa mambo wanaendelea kusema kwamba, Rio mwaka huu hapatoshi, kwani wanategemea
kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, atafunika! Kwani ameonesha upendo na matumaini makubwa
kwa vijana. Anawakumbusha kwamba, wao ndiyo furaha na chemchemi ya imani, kwa njia
ya uwepo wao Kanisa kamwe haliwezi kuzeeka. Ni changamoto ya kutumia karama na vipaji
walivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa na Jamii inayowazunguka.
Vijana
kamwe, wasiogope kuwa na ndoto kubwa na wasikubali baadhi ya watu kuwapokonya matumaini
yanayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao! Wawe na ujasiri wa kukumbatia zawadi
ya maisha. Kwa maneno machache Papa Francisko ameonesha umahiri mkubwa wa kuzungumza
na vijana, kwa kweli watu wanasubiri makali yake!
Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani nchini Brazil yanawahamasisha vijana kuwa na ari na moyo wa kimissionari.
Wasikilize kwa umakini mkubwa Katekesi na Mafundisho yatakayotolewa ili hatimaye,
waweze pia kuwashirikisha vijana wenzao. Neno la Mungu liwe ni dira na taa inayoangaza
mapito yao! Wasisahau kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho,
ili kuonja huruma na upendo wa Mungu. Fumbo la Msalaba liwakumbushe vijana: mateso,
kifo na ufufuko wa Kristo, kiini cha imani ya Kanisa.
Vijana wanapaswa kuonjeshwa
ushuhuda wa imani tendaji ili waweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa
lake. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni dawa inayoponya mchoko wa watu kuendelea
kuamini kwa kuamsha ari na moyo mpya wa Kimissionari, ambao unawawezesha vijana kuwa
ni vyombo madhubuti vya Uinjilishaji.
Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.