Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania litaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, ili
kuhakikisha kwamba, watanzania wanapata elimu bora, itakayowasaidia kupambana na changamoto
za maisha kwa ari na ujasiri mkubwa.
Hayo yamebainishwamwishoni mwa juma katika
hafla ya kuchangia Kituo cha Mwalimu Julius Nyerere, kilichoko kwenye Chuo Kikuu cha
Kikatoliki cha Afya na Sayansi Mwambata, Bugando, Mwanza. Kituo hiki kitakapokamilika,
kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 800. Ujenzi wa awamu ya kwanza unatarajiwa
kugharimu kiasi cha shilingi billioni 3/. Hiki kitakuwa ni kituo cha tafiti kinachotarajiwa
kuhudumia wadau mbali mbali katika sekta ya tiba na dawa nchini Tanzania.
Rais
mstaafu Benjamin William Mkapa wa Tanzania ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika uwekaji
wa jiwe la msingi la Kituo cha Mwalimu Julius Nyerere, CUHAS. Amewataka watanzania
kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea misingi ya haki, amani na utulivu nchini Tanzania.
Hizi ni tunu msingi zilizohubiriwa na kumwilishwa na Mwalim Nyerere katika maisha
na uongozi wake kama Rais wa Tanzania.
Naye Mheshimiwa Padre Charles Kitima,
aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT amesema, bila: haki, amani na utulivu,
hakuna maendeleo na kwamba, afya ya wananchi itasuasua tu: Kumbe, amani na utulivu
ni jina jipya la maendeleo ya mwanadamu kiroho na kimwili.