2013-07-12 07:37:20

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 15 ya Kipindi cha Mwaka C. wa Kanisa


Ninakuleteeni Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 15 ya Kipindi cha mwaka C wa Kanisa. Leo Mama Kanisa ametuwekea Neno la Bwana akitufudisha Amri kuu ya Mapendo yaani kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Mwinjili Luka anasema, Mungu ni mkuu mno kumbe kumpenda yeye lazima kujidhihirishe pia katika kumpenda jirani yetu. RealAudioMP3

Katika Injili ya Dominika hii jirani ni awaye yote mwenye taabu na masumbufu mbalimbali katika maisha. Ni yule anayehitaji msaada wako, asiye na chakula, asiye na mahali mahali pazuri pa kuishi. Bwana anatoa fundisho hili baada ya kuulizwa swali na mwanasheria juu ya namna gani aweza kuurithi uzima wa milele. Bwana akitambua hila yake anajibu swali hilo kwa kuweka swali mbele ya mwansheria na swali hilo linalala katika kile anachokifahamu mwanasheria huyu. Bwana anasema Torati yatufundisha nini juu ya hilo? Mwanasheria atajibu akisema mpende Bwana Mungu wako na jirani yako.

Baada ya jibu la mwanasheria Bwana akitambua yakuwa lazima fundisho lake likae katika mazingira halisia ili liweze kueleweka vema, anafundisha akitumia mfano wa Msamaria mwema. Basi Bwana anatoa mfano huo akianza na mtu mmoja ambaye hatumjui jina lake anayetelemka toka Yerusalemu kwenda Yeriko. Mtu huyu anavamiwa na wanyang’anyi na kuumizwa vyakutosha na anaachwa barabarani ambapo baadaye watapita watu wa aina mbalimbali walio katika makundi matatu. Mtu huyu kwa hakika huwakilisha wale wote walio katika taabu na mateso mbalimbali ya kiroho na kimwili katika maisha yao. Kisha kumweka mtu huyu katika mtililiko wa mafundisho yake ataweka sasa makundi ya watu wanaopita mahali ambapo mtu huyo alikuwa amesukumizwa kandokando ya barabara.

Mpendwa msikilizaji, kundi la kwanza na la pili yaani Kuhani na Mlawi yanaonesha hisia ileile na kundi la tatu yaani la Msamaria linaonesha hisia tofauti. Kundi la kwanza na la pili wanapita pale alipo mwenye taabu na hawaoneshi fikra yoyote yakutaka kumsaidia ndugu huyu mwenye taabu. Makundi haya mawili si kwamba hawana upendo bali wanafikiria na kuuona upendo kama jambo ambalo lazima likae katika mpango unaoendana na uchaguzi, maana yake wanachagua nani anasitahili huduma yao, kulingana na muda mwafaka na hata ikiwezekana kimahesabu.

Mpendwa, jambo hili ni la ajabu, upendo wawezaje kuwekwa katika vipimo vya kimahesabu na muda? Kwa hakika haiwezekani kuwa na jambo la namna hiyo. Kwa maana jirani si yule ambaye mara zote unamfahamu bali yule unayekutana naye pasipo kutarajia, ni yule anayepangua mipango yako ya maendeleo, ni yule anayejeruhi ratiba yako uliyoipanga! Kwa namna hiyo usemi huu waweza kuwa wa kweli “utampenda Bwana kwa uwepo wako wote na utampenda yule usiyemtarajia kama unavyojipenda mwenyewe”

Mpendwa msikilizaji, kundi la tatu ni lile la Msamaria mwema. Wote twatambua uhusiano kati ya Wayahudi na Wasamaria. Wasamaria mbele ya Wayahudi ni watu wasio na elimu, ni watu wa kutengwa na ni wazushi, kumbe ilikuwa lazima kuwaepuka. Ni katika mantiki hiyo basi Msamaria angekuwa wa kwanza kumkwepa huyu mteswa wa njiani!

Badala yake anasimama na kutoa huduma baada ya kuguswa moyoni mwake na taabu ya mwingine. Yeye haweki upendo katika mahesabu wala haangalii muda gani atapoteza anachotazama ni wokovu wa mtu huyu. Upendo huvumlia, upendo huaanza moyoni na humalizikia katika kutoa huduma. Msamaria huyu haishii katika kutenda peke yake bali anamshirikisha mwingine taabu hiyo,yaani mwenye hotel. Mpendwa mwana wa MUngu mwenye hotel anawakilisha mfumo wa kijamii ambao kama haupo huruma na upendo wetu hubaki katika ubinafsi pasipo kufikia lengo lake! Ni kwa namna hiyo basi mifumo jamii inahitaji kushtuliwa ili ukamilifu wa maisha ya mapendo uweze kufikia kilele chake.

Mpendwa msikilizaji wajifunza nini toka fundisho hili la Bwana? Wapi unatakiwa kufika baada ya kutafakari mfano huu? Kwa hakika lengo ni kutaka kukufikisha katika upeo wa kupambanua kuwa Msamaria mwema namba moja ni Yesu mwenyewe, ndiye amekuwa karibu na wateswa na maskini na wafungwa, akitaka kuwaondoa na amewaondoa kweli katika taabu zao. Lk 4:18. Basi nasi tukiwa wana wa Mungu twaitwa kujifungamanisha katika Bwana tukiyachuchumalia mafundisho hayo ya Bwana. Nikutakie yote mema katika kujitahidi kuwa Msamaria mwema.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.