Tanzania itafaidika na mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaogharamiwa na Serikali
ya Sweden utakao gharimu kiasi cha T.Shs trilioni 1.4 kupitia kitengo chake cha Swedish
International Cooperation Agency (SIDA). Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mheshimiwa
Lennarth Hjelmaker amemueleza Rais Jakaya Kikwete Ikulu ambapo alifika kumkabidhi
Rais barua kutoka kwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Sweden Mheshimiwa Gunilla
Carlsson, ambaye amemwandikia Rais Kikwete barua maalum kumjulisha kuhusu mpango huo
ambao Serikali ya Sweden utaugharamia.
Mpango huo wa maendeleo wa 2013-2019
unalenga katika maeneo makuu matatu: ·Kuongeza ajira, kuendeleza sekta ya nishati
na masoko kwa mazao ya kilimo; ·Elimu ambapo kipaumbele kitakuwa katika kuwapa
elimu ya awali watot wengi zaidi na pia katika vyuo vya ufundi; ·Kukuza demokrasia,
uwajibikaji na uwazi pamoja na kuongeza uelewa wa haki za binadamu nchini.
Katika
barua yake kwa Rais Kikwete, Waziri Carlsson amemueleza Rais Kikwete kuwa Tanzania
itaendelea kuwa mwenza muhimu kwa nchi ya Sweden “Huu si ushahidi wa ushirika wetu
wa kihistoria, bali pia ni kwa ajili ya sera za Tanzania na ukuaji wa taasisi za
kidemokrasia nchini Tanzania” amesema Waziri Carlsson na kuongeza kuwa “Wakati uhusiano
baina ya nchi hizi mbili ni muhimu, mahusiano yetu ya baadaye yataimarika zaidi sio
kwenye misaada bali katika uwekezaji” ameongeza.
Rais Kikwete ameishukuru
Sweden kwa msaada huo na kueleza kuwa nchi zinazoendelea kwa hakika zinahitaji misaada
ya maendeleo ili kujijengea uwezo na hatimaye, kufikia kwenye uwekezaji ambao utaharakisha
maendeleo ya nchi hizi.