Padre ni Mwalimu wa mambo ya Kimungu, Kuhani anayeadhimisha Mafumbo ya Kanisa na Mchungaji
mwenye moyo wa upendo na huruma!
Katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Benedikto Abate, hapo tarehe 11 Julai
2013 ambaye katika Kanuni za maisha ya kitawa alikazia sala na kazi, Jimbo Katoliki
la Dodoma, limemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Maadhimisho ya
Miaka 17 tangu Askofu Gervas Nyaisonga alipopewa Daraja Takatifu la Upadre. Waamini
wanamwombea ili aendelee kuwafundisha, kuwatakatifuza na kuwaongoza kadiri ya moyo
na mapenzi ya Kristo, Mchungaji mkuu.
Askofu mstaafu
Mathias Isuja wa Jimbo Katoliki la Dodoma, alitoa Sakramenti ya Daraja takatifu la
Upadre kwa Shemasi Laurent Lelo baada ya kuhitimu masomo na majiundo yake ya Kipadre:
Seminari kuu ya Ntungamo iliyoko Jimbo Katoliki la Bukoba na Kipalapala iliyoko Jimbo
kuu la Tabora. Itakumbukwa kwamba, alipewa Daraja la ushemasi hapo tarehe 13 Januari
2013 na Askofu mstaafu Mathias Joseph Isuja.
Askofu mstaafu Isuja anasema,
Shemasi Laurent Lelo anapewa Daraja Takatifu la Upadre, wakati huu wa ukame wa miito
ya Kipadre, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani unaoendelea kuibua changamoto
mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mwaliko wa kuendelea kusikiliza sauti
ya Kristo anayesema kwamba, mavuno ni mengi, lakini watenda kazi katika shamba la
Bwana ni wachache, basi waendelee kumwomba Bwana wa mavuno ili apeleke watenda kazi,
wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba lake.
Askofu mstaafu Isuja, amemkumbusha
Shemasi Lelo kwamba, ameitwa, akatakaswa na kutumwa na Mwenyezi Mungu kutangaza Habari
Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Yeye anashiriki Nafsi ya Kristo kwa kuwa: kuhani,
mwalimu na mchungaji. Anapaswa kuwa ni Kuhani kwa mfano wa Melkisedeki aliyekuwa mchamungu
na mtu wa amani. Kama Padre anatumwa kuwa mwalimu wa mambo ya Kimungu na wala si "kufundisha
sera zake", ndiyo maana anapaswa kulifahamu, kuliishi na kulitangaza Neno la Mungu.
Kama
Padre anatumwa kuwatakasa watu kwa njia ya Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, kamwe
watu wasitindikiwe na neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kwa vile tu, Padre
amemezwa na malimwengu hana muda wa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa.
Kama Mchungaji
kwa moyo na ari ya Kristo anapaswa kujivika huruma na upendo kwa kuzikabili changamoto
za ulimwengu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha adili. Aendelee
kumtegemea Roho Mtakatifu atakayemkirimia matunda ya Roho Mtakatifu kama yalivyobainaishwa
kwenye Maandiko Matakatifu.