2013-07-12 08:01:18

Kanisa linapania kulinda na kudumisha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu!


Kanisa lina wajibu na dhamana ya kushiriki katika maisha ya Jamii inayolizunguka, kwani linatumwa kumhudumia mtu mzima kiroho na kimwili na kwamba, ushiriki wake katika masuala nyeti ya kijamii linapania kulinda na kudumisha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. RealAudioMP3

Kanisa linatambua na kuheshimu tofauti kati ya Kanisa na Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake kama zinavyofafanuliwa na Katiba ya nchi ambayo kimsingi ndiye sheria mama!

Ufafanuzi huu umetolewa hivi karibuni na Askofu msaidizi Broderick Pabillo wa Jimbo kuu la Manila wakati akichangia mada tete kuhusu Kanisa kuingilia masuala ya kisiasa na kwamba, Kanisa lilikuwa halina haki ya kufanya hivi, bali kujikita katika kuhubiri Injili Makanisa tu! Anasema, viongozi wa Kanisa wanaposhiriki katika mijadala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, kwanza kabisa wanatekeleza wajibu wao kama raia wa nchi na pili kama viongozi wa Kanisa wanaomhudumia mwanadamu mzima: kiroho na kimwili.

Wanayo haki ya kupongeza pale Serikali inapotekeleza vyema wajibu wake msingi kwa raia wake, lakini pia viongozi wa Kanisa wanayo haki na dhamana fungamanishi inayowataka kusema wazi, wakisukumwa na ukweli, mafao ya wengi, utu na heshima ya mwanadamu, umoja na mafao ya wengi. Ikiwa kama viongozi wa Kanisa watakaa kimya na kufumbia macho mabaya yanayotendeka ndani ya Jami watakuwa ni wanafiki na watu wasiotekeleza wajibu wao barabara.

Viongozi wa Kanisa wanatambua kwamba, wao ni sauti ya kinabii, inayowakilisha wale wasiokuwa na sauti katika Jamii, kumbe mchango wao unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na pale inapowezekana ufanyiwe kazi kwa ajili ya mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi. Mafundisho Jamii ya Kanisa ndiyo dira na mwongozo katika kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Haya ni masuala nyeti yanayowagusa watu wa imani na dini mbali mbali na wala si kwa ajili ya Waamini wa Kanisa Katoliki.

Kuhusu sheria ya uzazi salama, ambayo imekuwa ni chanzo cha kinzani na misigano kati ya Serikali ya Ufilippini na Kanisa Katoliki ni pale ambapo sheria inakumbatia sera za utoaji na vizuia mimba kama njia ya kuratibu ongezeko la watu nchini Ufilippini. Baraza la Maaskofu Katoliki linawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutumia njia za mpango asili wa uzazi kama sehemu ya mchakato wa kusimama kidete kupinga utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za uzazi salama.

Maaskofu wanasema ndoa kati ya mume na mke ni jambo takatifu na la kudumu, ikiwa kama sheria na taratibu zote zimezingatiwa. Serikali kwa upande wake, inataka kutoa ruksa kwa wanandoa kutalakiana ikiwa kama mambo hayaendi vyema ndani ya familia zao.

Serikali na Kanisa wanapotekeleza wajibu na dhamana yao wanawahudumia wananchi wa Ufilippini, licha ya imani na misimamo yao ya kidini. Kanisa litaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchi, litasimama kidete pia kutetea Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya mafao ya wengi ndani ya Jamii.

Ni wajibu wa kila mwananchi kuongozwa na dhamiri nyofu, ambayo kimsingi ni sheria ya Mungu iliyoandikwa katika moyo wa mwanadamu inayompatia nafasi ya kutambua jambo jema la kufuata na baya ambalo linapaswa kuhepukwa. Ni wajibu wa waamini walei kwa njia ya ushuhuda wa maisha na imani yao, kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwani ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaweza kumfanya mwanadamu akapoteza dira na mwongozo wa maisha. Ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kushikamana na Kristo pamoja na Kanisa lake.








All the contents on this site are copyrighted ©.