Mabadiliko ya Sheria za makosa ya jinai na kazi yatolewa mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko kwa utashi wake mwenyewe, tarehe 11 Julai 2013 amefanya mabadiliko
katika baadhi ya sheria za makosa ya jinai na adhabu katika makosa ya kiutendaji ambazo
zimekuwa zikitumika mjini Vatican. Sheria ambazo zilikuwa zikitumika kwa ajili ya
Tume ya Kipapa ya Mji wa Vatican, sasa zitaanza kutumika katika shughuli zote zinazotekelezwa
na Vatican.
Sheria hizi mpya ni mwendelezo wa mageuzi ya sheria za Vatican
yaliyoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kunako mwaka 2010.
Hizi ni sheria ambazo kwa sasa zinakidhi viwango vya kimataifa pamoja na kuzingatia
itifaki ya Mwaka 1949 kuhusu vita na makosa ya kivita. Itifaki ya mwaka 1965 kuhusu
ufutwaji wa aina zote za ubaguzi wa rangi; itifaki ya mwaka 1984 inakataza mateso
na ukatili dhidi ya binadamu na adhabu kali; Itifaki ya mwaka 1989 inabainisha kuhusu
haki za mtoto pamoja na itifaki ya mwaka 2000.
Sheria hizi zinafafanua kwa
kina kuhusu makosa dhidi ya ubinadamu, kwa kujikita zaidi katika: mauaji ya kimbari
mintarafu ufafanuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa. Kumefanyika pia marekebisho
ya sheria dhidi ya makosa yanayotendwa na mtu anapokuwa kazini mintarafu mikakati
ya Umoja wa Mataifa kupambana na rushwa. Adhabu ya kifungo cha maisha imefutwa na
badala yake adhabu ya juu itakuwa ni kati ya miaka 30 hadi 35 jela.
Sheria
mpya zinawabana wafanyakazi wa mahakama wanaoweza kujinufaisha kwa nafasi na madaraka
waliyonayo katika vituo vyao vya kazi. Katika mfumo mzima wa sheria, jambo la kwanza
katika mchakato huu ni mhusika atahesabiwa kuwa ni mtuhumiwa hadi pale itakapobainika
kwamba, ametenda kosa. Mahakama imepewa madaraka ya kuweza kutaifisha mali ya watuhumiwa.
Sheria zinazohusu ushirikiano wa kimataifa zimeboreshwa kwa kuzingatia itifaki za
kimataifa zilizotolewa hivi karibuni.
Sheria na adhabu kuhusu utekelezaji wa
majukumu zina asili ya jumla, ili kutoa mwelekeo wa jumla kuhusu adhabu zinazoweza
kutolewa katika maeneo mbali mbali, kama njia ya kuhakikisha kwamba, sheria na mafao
ya Jamii yanalindwa. Kimsingi, sheria hizi zinapania pamoja na mambo mengine kuboresha
mfumo wa sheria za Vatican kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kuongeza tija na
ufanisi.