2013-07-11 11:21:01

Kardinali Pengo atema cheche DRC!


Ni matumaini ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika na Madagascar, SECAM kwamba, DRC ambayo hivi karibuni imeadhimisha Uhuru wake, itaendelea kudumisha msingi wa haki, amani na ustawi wa wananchi wake. SECAM ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, iliyoanzishwa ili kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha, utume na ustawi wa Kanisa Barani Afrika.

Ni chombo kinachojihusisha na mchakato wa ujenzi wa Familia ya Mungu Barani Afrika, kwa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na inaundwa na Mataifa 38 yanayowakilishwa kwenye Mashirikisho ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika. Licha ya matatizo na changamoto mbali mbali, SECAM imeendelea kuwa ni chombo makini cha Uinjilishaji Barani Afrika, hasa kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho. SECAM inawajibu wa kuendelea Kuinjilisha katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kumi na sita wa SECAM, hapo tarehe 9 Julai 2013 mjini Kinshasa, DRC. kwa kujikita zaidi na masuala ya haki, amani na upatanisho. Kanisa linapania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili, hali inayojionesha kwa namna ya pekee katika huduma za elimu, afya na maendeleo endelevu, hasa miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Kardinali Pengo anasema, ukosefu wa amani na utulivu unakwamisha kwa kiasi kikubwa mchakato wa Uinjilishaji Barani Afrika unaopania kwa njia ya haki, amani na upatanisho, kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, ili kuwawezesha Waafrika kucharuka katika maendeleo katika sekta mbali mbali za maisha. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake, Dhamana ya Afrika, analitaka Kanisa Barani Afrika kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kiulimwengu kutokana na amana zilizohifadhiwa katika maisha na mioyo ya waamini Barani Afrika.

Katika kipindi cha Miaka 50 iliyopita, Bara la Afrika limejikuta likikabiliwa na utawala mbovu; rushwa na ufisadi; vita, kinzani za kidini, kikabila na kimajimbo, mambo ambayo yamepelekea athari kubwa kwa maisha na ustawi wa wananchi wa Bara la Afrika. Kuna baadhi ya watu wameendelea kujineemesha na utajiri pamoja na rasilimali za Bara la Afrika kwa mafao yao binafsi. Huu ni ukiukwaji wa haki msingi, maadili na utawala wa sheria; mambo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa!

Kinzani za kisiasa na vita, umekuwa ni wimbo usiokuwa na msikilizaji katika maeneo ya Maziwa Makuu, Sudan ya Kusini, Darfur, Afrika ya Kati, Kaskazini na Mali. SECAM inapenda kuwahamasisha waamini na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na kijamii kama sehemu ya mchakato unaopania kujenga ufalme wa Mungu, unaosimikwa katika: haki, amani na upendo kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi, mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa.

SECAM imeendelea kukazia misingi ya utawala bora, ndiyo maana inatafuta uwakilishi kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa, ili kuweza kushirikisha mchango wa Kanisa Barani Afrika katika mapambano dhidi ya: umaskini, ujinga, maradhi, uharibifu wa mazingira pamoja na kushiriki katika mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kukazia utawala bora, demokrasia na matumizi bora ya rasilimali ya Bara la Afrika.

Kardinali Pengo ameyashukuru Mabaraza ya Makanisa Barani Afrika kwa kuendelea kushirikiana na SECAM katika kukabiliana na changamoto za Bara la Afrika. Ni matumaini yake kwamba, kwa pamoja wanaweza kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kupambana na changamoto hizi, ikiwa ni pamoja na Kikundi cha Boko haram ambacho kwa sasa kimekuwa ni tishio kwa amani na usalama wa watu nchini Nigeria.

Ni wajibu wa viongozi kusaidia kukuza na kudumisha misingi ya maadili na utu mwema miongoni wa vijana, wanaokabiliwa na kasi kubwa ya kumong'onyoka kwa maadili. Bara la Afrika linapaswa kujenga miundo mbinu thabiti ili kufurahia rasilimali ya dunia, badala ya kuendelea kutegemea ufadhili!

Mkutano huu unahudhuriwa pia na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Askofu mkuu Tito Llyana, Balozi wa Vatican nchini DRC; wawakilishi wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika, Mapadre na Watawa.







All the contents on this site are copyrighted ©.