Ifuatayo ni Hhotuba ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika kilele cha sherehe za kuadhimisha
miaka 50 ya Jeshi la Kujenga Taifa Uwanja wa Uhuru, 10 Julai, 2013 Jijini Dar es salaam.
Pongezi
Nakushukuru sana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja
Jenerali Raphael Muhuga kwa kunishirikisha kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka
50 ya uhai wa Jeshi la Kujenga Taifa. Nawapongeza sana kwa maandalizi mazuri ya sherehe
hizi ambazo hakika zimefana sana. Gwaride lilikuwa zuri na tumeburudika vya kutosha
kutoka vikundi vya ngoma, ngonjera na nyimbo. Kwa niaba yangu, ya Serikali na
ya Watanzania wote nawapongeza kwa dhati Maafisa Wakuu, Maafisa Wadogo, wapiganaji
na vijana wa JKT popote pale walipo kwa kusherehekea Jubilei ya Dhahabu ya uhai wa
JKT. Mnastahili kuwa na furaha na kusherehekea kama tulivyoshuhudia sote.
Historia
ya JKT
Ndugu Wananchi; Miaka 50 iliyopita, tarehe kama ya leo, yaani
tarehe 10 Julai, 1963 Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa rasmi. Huu ulikuwa ni utekelezaji
wa Azimio la Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika tarehe 19 Aprili, 1963 chini
ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika. Wazo la kuanzishwa kwa JKT lilitokana na mapendekezo ya busara ya Mkutano
Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU Youth
League), uliofanyika mkoani Tabora mwaka 1958. Wazo hili lilitolewa na Katibu Mkuu
wa TANU Youth League wakati ule Ndugu Joseph Nyerere ambaye sasa ni marehemu. Lengo
kuu la kutaka kuundwa kwa JKT lilikuwa ni kuwandaa vijana kuwa raia wema, wawe na
moyo wa uzalendo, na wawe tayari kulitumikia taifa lao kwa nguvu na uwezo wao wote.
Ndugu Wananchi; Jeshi la Kujenga Taifa lilianza na Vijana 11 kutoka
Wilaya 11 nchini. Hao ndio walikuwa wa kwanza kupata mafunzo katika Kambi ya JKT
Mgulani, Jijini Dar es Salaam. Vijana hao walikuwa ni Makatibu wa Umoja wa Vijana
wa TANU na wengine walimu. Niruhusuni niwatambue watu hao kuwa ni Bi Zainabu Kiango,
Bw. Sebastian Chale, Bw. Peter Lwegarulira, Bw. Rupho Kamba, Bw. Hashim Ngaliwason,
Bw. John Ndimugangwo, Bw. Said Desai, Bw. Dismas Msilu (Brigedia Mstaafu), Bw. Athumani
Msonge (Brigedia Jenerali Mstaafu), Bw. Reginald Mitande na Bw. Eslei Mwakyambiki.
Kati ya hao 11, walio hai ni Bi Zainabu Kiango na Brig. Jenerali Dismass Msillu
ambao wapo nasi siku ya leo. Waliosalia wameshatangulia mbele ya haki. Mwenyezi
Mungu awarehemu. Kundi la pili liliwajumuisha Bi. M. Mhando, Bw. E. Simkone, Bw.
Mwanimlele (Asst Master) Bw. AA Moyo (Asst Master) ambao walijiunga na kupata mafunzo
ya uongozi.
Sheria Iliyoanzisha JKT
Ndugu Wananchi; Mwaka
1964, Bunge lilitunga Sheria ya Kuanzisha JKT iliyoupa nguvu ya kisheria uamuzi wa
mwaka 1963 wa Baraza la Mawaziri wa kuanzishwa kwa Jeshi hilo. Kwa mujibu wa Sheria
ile, kujiunga na JKT ilikuwa jambo la kujitolea kwa mapenzi ya mtu. Lakini mwaka 1966,
Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuanzisha utaratibu wa kujiunga na JKT kwa mujibu
wa Sheria.
Utaratibu huu uliwahusu vijana waliohitimu vyuo vikuu, vyuo vya
elimu ya juu, kidato cha sita na waliomaliza kidato cha nne ambao wamepata mafunzo
kwenye vyuo vya taaluma mbalimbali kama vile ualimu, uganga, uuguzi na kadhalika.
Mkurugenzi wa JKT aliwezeshwa kisheria kuwaita vijana hao kujiunga na JKT. Mwezi
Julai 1967, kikundi cha kwanza cha vijana wasomi 64 kilijiunga na JKT katika Operesheni
Azimio.
Katika kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu kuanzishwa
kwa Jeshi la Kujenga Taifa, viongozi na wasomi wengine waliohitimu zamani waliamua
kujiunga na mafunzo ya JKT. Mwezi Januari, 1968, kwa mfano, aliyekuwa Makamu wa Pili
wa Rais, Mheshimiwa Rashid Kawawa, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza
wa Rais, Mheshimiwa Aboud Jumbe, aliyekuwa Spika wa Bunge Chifu Adam Sapi Mkwawa pamoja
na baadhi ya Wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali walijiunga na mafunzo
ya Jeshi la Kujenga Taifa. Wote walikuwa katika kambi ya Ruvu ambapo walipatiwa mafunzo
ya uongozi.
Ndugu Wananchi; Mwaka 1975 JKT iliunganishwa na Jeshi la Ulinzi
la Wananchi wa Tanzania na hivyo kuwa sehemu kamili ya JWTZ. Kuanzia wakati ule,
Maafisa na Askari wa JKT wakawa ni wa JWTZ na kutambulika kwa vyeo vya JWTZ. Jeshi
la Kujenga Taifa liliendelea na majukumu yake ya kutoa mafunzo kwa vijana wa kujitolea
na wa mujibu wa sheria. Hata hivyo, mambo mawili ya msingi yalisisitizwa au kuongezwa
katika majukumu ya JKT. Kwanza kwamba, kuwa Divisheni ya Uzalishaji ya JWTZ yenye
dhamana ya kulipatia Jeshi mahitaji yake ya chakula, mavazi na mengineyo. Pili, kwamba
JKT ndipo mahali pa kutolea mafunzo ya awali ya kijeshi na kwamba JWTZ itaajiri kutokana
na wanaohitimu JKT.
Katika dhamira ya kutimiza wajibu wa kwanza kwa ufanisi,
mwaka 1982 Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT) liliundwa. Shabaha kuu ilikuwa
ni kuwa na chombo madhubuti cha kupanga, kusimamia, kuratibu na kutekeleza majukumu
ya uzalishaji mali na kiuchumi katika JKT kazi ambayo shirika linaendelea kuifanya
hadi sasa.
Kusitishwa kwa Mafunzo ya JKT
Ndugu Wananchi Tunapoangalia
nyuma, katika historia ya miaka 50 ya kuzaliwa na uhai wa JKT tunaona wazi kuwa yamepatikana
mafanikio makubwa. Tena ni mafanikio ya kutia moyo na kujivunia. Ninaposema hivyo,
napenda nisieleweke vibaya kuwa sitambui ukweli kwamba kulikuwepo vipindi vigumu vyenye
changamoto za namna mbalimbali. Zilikuwepo changamoto kubwa na ndogo na zilizokuwa
ngumu na nyepesi kuzipatia ufumbuzi. Aidha, natambua kuwa bado zipo changamoto kadhaa
tunazoendelea kukabiliana nazo. Jambo la msingi na la faraja ni kwamba pamoja na
changamoto hii tumefanikiwa sana.
Ndugu Wananchi; Kwa upande wa mafunzo
kwa vijana, kwa mfano, zaidi ya vijana 305,625 wamepitia JKT na kupatiwa mafunzo ya
kijeshi na ya stadi mbalimbali za maisha katika fani na nyanja mbalimbali. Tangu
mwaka 1963 mpaka sasa yameshapita makundi (kwa jina maarufu Operesheni) 102.
Bahati
mbaya kwa sababu ya hali mbaya ya uchumi iliyoikabili nchi yetu kuanzia nusu ya pili
ya miaka ya 1970 na kuwa mbaya zaidi miaka ya 1980 na mwanzoni mwa 1990, hali ya utoaji
wa mafunzo kwa vijana katika JKT iliathirika sana. Upatikanaji wa huduma na mahitaji
kwa ajili ya mafunzo na kuendesha kambi na JKT kwa jumla ukawa mgumu.
Pengine
ni vyema nikaeleza kuwa kupanda sana kwa bei ya mafuta duniani, kuanguka kwa bei za
mazao yetu tunayouza nje na gharama kubwa ya vita dhidi ya Idi Amin wa Uganda ndivyo
vilivyosababisha uchumi wa nchi yetu kutetereka. Hali hii ilipunguza sana uwezo
wa Serikali kutimiza majukumu yake ya msingi katika sekta, karibu zote nchini.
Ndugu
Wananchi; Kwa sababu hiyo, kwa upande wa JKT mwaka 1993, Serikali ililazimika kusimamisha
mafunzo kwa vijana wa kujitolea na mwaka 1994 ilifanyika hivyo kwa vijana wa mujibu
wa Sheria. Kwa kweli baada ya mwaka 1994 shughuli za msingi za JKT zilidorora sana
na kubakiza za kulinda kambi na zile Shirika la Uchumi (SUMAJKT). Hata hizo nazo
hazikuwa zinafanyika kwa kiwango kikubwa wala hazikuwa kwa ufanisi mkubwa kwa sababu
ya kutokupata fedha za kutosha kutoka Serikalini. Fedha za uendeshaji wa shughuli
zake zilikuwa kidogo.
Ndugu Wananchi; Kuifufua JKT ilikuwa ni
moja ya mambo niliyoyapa kipaumbele cha juu nilichojiwekea katika mipango ya kazi
baada ya kupewa heshima kubwa ya kuliongoza taifa letu Desemba 21, 2005. Mtakumbuka
kuwa katika hotuba yangu ya kuzindua Bunge tarehe 30 Desemba, 2005, nilipozungumzia
kufanya kila tuwezalo kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana, nilikuwa
nazungumzia kufufua na kuimarisha Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na kuwepo kwa shule
za kitaifa hasa za sekondari.
Ni ukweli ulio wazi kwamba JKT imefanya kazi
kubwa na nzuri ya kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia
Jeshi hilo. Hapa ni mahali ambapo vijana wa rangi zote, makabila yote, dini zote
hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa nchi moja. Hakuna
chombo chochote cha malezi ya vijana kilichoizidi JKT katika kazi hiyo. Kwangu mimi
na wenzangu katika Serikali ninayoiongoza kufufua mafunzo ya vijana wa kujitolea na
mujibu wa sheria lilikuwa suala kubwa na muhimu sana kulitekeleza.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri sikuwa peke yangu mwenye fikira na matamanio hayo. Watu wengi ndani
ya Serikali, nje ya Serikali na miongoni mwa raia na Bungeni walikuwa wanaunga mkono
mawazo hayo. Sababu kubwa ni kuwa athari za kusimamishwa mafunzo ya JKT ziliwagusa
wengi na ndiyo maana kumekuwepo na madai ya kutaka mafunzo yarudishwe.
Kule
Bungeni kauli yangu kuhusu JKT iligeuka kuwa deni kubwa kwangu na kwa Serikali. Madai
ya kutaka Serikali irejeshe mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yalikuwa yanajitokeza
mara kwa mara na mwangi wake ulikuwa unaongezeka ukali kila mwaka. Nafurahi kwamba
hatimaye tarehe 26 Machi, 2013 tulifanikiwa kutimiza dhamira na ahadi yetu nilipozindua
kuanza upya kwa mafunzo hayo katika kambi ya Ruvu. Kundi la kwanza limemaliza mafunzo
yake na la pili limeshafika katika makambi na tayari wameanza mafunzo.
Kama ilivyokuwa mwaka 1964 JKT ilipoanza, na mwaka 1968 baada ya mafunzo ya mujibu
wa Sheria kuanzishwa, viongozi wa kitaifa waliongoza kwa mfano; safari hii Wabunge
wetu alionesha. Mwaka huu Wabunge 22 wamefanya na kumaliza mafunzo ya uongozi. Baadhi
yao wako nasi siku ya leo. Niruhusuni nirudie kutoa pongezi zangu za dhati kwao kwa
kuwa viongozi wa mfano.
Ndugu Wananchi; Taarifa nilizonazo
ni kuwa wamefanya na kumaliza mafunzo yao vizuri. Walikuwa na nidhamu nzuri, utii
na moyo wa kujituma. Wamemaliza wakiwa ni askari wakakamavu na wenye mtazamo mpya
na bora zaidi kuhusu masuala ya utaifa, uzalendo na mustakabali wa taifa letu na watu
wake.
Ndugu Wananchi; Kwa upande wa shughuli za kiuchumi zinazofanywa
na JKT tuliazimia kuwa, tutafanya kila tuwezalo kuimarisha SUMAJKT. Tumefanya mambo
kadhaa kwa ajili hiyo na tumekuwa tunapata mafanikio ingawaje bado tunayo safari ndefu
ya kulijenga shirika hili mpaka liwe bora kwa shughuli lizifanyazo. Naamini tutafika
pale tunapopatarajia.
Tuliamua kutoa upendeleo maalum kwa JKT kwa kutoa
shughuli na miradi kadhaa ya Serikali waitekeleze wao. Kwa mfano, ujenzi wa nyumba
na majengo kadhaa ya Serikali pamoja na ujenzi wa barabara, mabwawa ya maji na miradi
ya kilimo cha umwagiliaji na kadhalika. Tumewapa JKT kazi ya kuzalisha mbegu bora
kwa wakulima. Vile vile, Serikali imechukua mkopo wa dola za Marekani milioni 40
kutoka Serikali ya India uliotumika kununua matrekta 1,846 kutoka Serikali ya India
na kuipa SUMAJKT kuuza kwa wakulima kama biashara yao.
Hivi sasa mchakato
unaandaliwa wa kupata mkopo mwingine wa dola za Marekani milioni 92 kwa ajili hiyo.
Tumefanya yote hayo kwa makusudi mazima ya kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kuwa
na shirika lililoimara na linalotekeleza kwa ufanisi majukumu yake. Halikadhalika
itawezesha JKT kudumisha sifa yake nzuri katika kilimo, ufugaji, uvuvi na ujenzi.
Ndugu
Wananchi; Napenda kuchukua nafasi hii, kuwashukuru kwa dhati ya moyo
wangu, Wakuu wa JKT kumi, waliotangulia pamoja na Meja Jenerali Muhuga aliyepo sasa.
Tunawapongeza kwa utumishi wao uliotukuka na moyo wao wa upendo kwa nchi yetu na watu
wake. Mafanikio haya tunayojivunia leo yametokana na juhudi kubwa za viongozi hawa
wakishirikiana na maafisa, askari na wafanyakazi raia katika kubuni na kusimamia utekelezaji
wa shughuli za JKT. Mimi na Watanzania wenzangu wote hatuna neno lingine zuri
la kuwaonesha upendo wetu na shukrani zetu zaidi ya kusema asanteni sana. Tunatambua
na kuthamini mchango wenu. Tutauenzi daima.
Changamoto na Dira
Mheshimiwa
Waziri; Pamoja na mafanikio ya kutia moyo, naelewa kuwa bado safari iliyo
mbele yetu ni ndefu na imejawa na changamoto nyingi ambazo hatuna budi kuzipatia majawabu.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa makazi ya maafisa na askari, upungufu
wa wataalamu katika miradi mbalimbali, upungufu wa vitendea kazi na vyombo vya usafiri.
Baadhi ya makambi hayana miundombinu mizuri ya kutoa kwa uhakika huduma muhimu kama
vile maji, umeme na kadhalika.
Napenda kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea
kushirikiana na JKT katika kutafuta njia mbalimbali za kuzipatia ufumbuzi changamoto
hizo. Tutaendelea kuongeza bajeti ya JKT kila mwaka na kuidhamini SUMAJKT ipate mikopo
ya kutekeleza miradi yake na shughuli zake. Tutaendelea kutoa upendeleo kwa Jeshi
na JKT katika kutekeleza baadhi ya miradi ya Serikali. Hata hivyo, nawaomba mzingatie
ubora wa kazi muifanyayo ili kulinda heshima ya JKT na kutulinda sisi tunaoamua kuwapa
upendeleo.
Ndugu Wananchi; Tunafanya haya kwa dhamira moja kubwa ya kutaka
kulifufua Jeshi la Kujenga Taifa na kulifikisha mahali panapostahili na kuwa chombo
madhubuti cha kutumainiwa na taifa. Nataka JKT liwe Jeshi la kisasa zaidi, linaloenda
na wakati na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu. Tunapenda mafunzo
yanayotolewa kwa vijana wanaojiunga na JKT yaendeshwe vizuri. Tunataka JKT itoe wazalendo
wa kweli, wanaothamini utaifa, umoja na mshikamano wa Watanzania. Vijana wanaopenda
kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea. Tunataka JKT izalishe askari walio
hodari na wanaoweza kulinda nchi yao kwa ujasiri mkubwa. Aidha, wanapoajiriwa na
vyombo vya ulinzi na usalama na kwingineko, idhihirishe wazi kuwa vijana waliopitia
JKT ni bora. Ni watu walioiva, wa kuaminika na kutumainiwa.
Hali kadhalika,
kwa wale wanaorudi uraiani kufanya shughuli nyingine wawe ni watu waliokamilika na
wenye uwezo wa kusimama wenyewe na kuendesha maisha yao. Kinachotakiwa ni kuwepo
kwa utaratibu mzuri kuwasaidia wanaojiajiri waweze kuanzisha shughuli za kuwaingizia
mapato kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyoyapata. Namna ya kuwawezesha vijana wanaomaliza
JKT waanze maisha ya kujitegemea ni jambo ambalo hatuna budi kulitafakari. Lakini
leteni mapendekezo yenu tuone namna ya kuyatekeleza.
Ndugu Wananchi; Mpaka
sasa bado JKT haijafanikiwa ipasavyo kuwa divisheni ya uzalishaji ya JWTZ kama ilivyotarajiwa.
Bado haizalishi chakula cha kutosheleza mahitaji ya JWTZ. Aidha, bado hawajaweza
kutosheleza mahitaji mengine ya JWTZ kama vile mavazi na kadhalika. Sasa wakati umefika
wa kujipanga vizuri kutekeleza jukumu hilo. JKT itumie sherehe hizi kufunga nadhiri
ya kupanga na kuanza safari ya dhati ya kufanya hivyo. Lakini, wasiishie hapo tu,
JKT iweke nia ya kuzalisha ziada ya kuuza nchini na hata nje ya nchi. Inawezekana,
jipangeni vizuri ili mtimize wajibu wenu. Rai kwa Makamanda wa JKT
Ndugu
Mkuu wa JKT, Makamanda, Maafisa na Askari; Ni jambo linalotia faraja
kubwa kwamba sote tunatambua kuwa katika miaka 50 iliyopita Jeshi la Kujenga Taifa
limepata mafanikio ya kutia moyo ingawaje safari ilikuwa na vikwazo mbalimbali. Hata
huko mbele muendako hatutegemei kuwa mambo yatakuwa rahisi, changamoto mbalimbali
zitaendelea kujitokeza. Hivyo basi, kinachohitajika ni kuendelea kuwa wabunifu kufanya
kazi ya ziada, tena kwa bidii zaidi, maarifa na moyo wa kujituma na kujitolea. Hizi
ni sifa ambazo mnazo, hivyo naomba muendelee kuzidumisha na kuziendeleza.
Endeleeni kuwa chuo mahiri cha kuwafunda vijana wetu wawe na moyo wa utaifa, uzalendo,
kujituma na kupenda kufanya kazi. Wawe raia wema na wawe tayari kutoa mchango stahiki
katika kujenga taifa lao. JKT inategemewa kuendelea kuwa kitovu cha shughuli za uzalishaji
mali, mafunzo ya stadi za kazi na ujasiriamali kwa vijana wetu. Endeleeni kuimarisha
JKT.
Nawaomba mtimize wajibu wenu huo kwa ukamilifu. Msituangushe. Nawaomba
endeleeni kuwa na moyo wa kuchapa kazi, muwe makini na waaminifu katika utendaji
wenu wa kazi za kila siku. Tafadhali zingatieni sana viapo vyenu vya utumishi jeshini
kwa kila ngazi ya uongozi. Muwe na nidhamu siku zote kama mwanajeshi anavyotakiwa
kuwa. Mkifanya hivyo, nina imani kuwa katika miaka michache ijayo JKT itapiga hatua
kubwa ya maendeleo. Taifa litanufaika sana.
Shukrani kwa Israel
Ndugu
Wananchi; Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitatambua na kuwashukuru marafiki zetu
wa Israel. Nchi ya Israel ndiyo iliyotupatia wakufunzi wa kwanza waliotusaidia katika
kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa. Aidha, walitoa mafunzo kwa viongozi wetu kadhaa
waasisi wa JKT nchini Israel. Serikali ya Israel imewakilishwa hapa leo na Balozi
wake nchini Mheshimiwa Gril Haskel. Naomba Balozi atufikishie salamu zetu nyingi
za shukrani kwa Rais Shimon Peres, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na watu wote wa
Israel kwa mchango wao muhimu walioutoa katika kuanzisha na kujenga Jeshi la Kujenga
Taifa. Hatasahau kamwe.
Mwisho
Ndugu Wananchi;
Mwisho, nawashukuru, kwa mara nyingine tena, Mheshimiwa Waziri Shamsi Nahodha na Meja
Jenerali Muhuga kwa kunialika. Nawashukuru wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali
na wa vyama vya siasa kwa kuja kwa wingi kushiriki katika sherehe za siku ya leo.
Na, kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi wote waliotembelea maonesho ya shughuli
zinazofanywa na JKT. Mmejionea wenyewe na kusikia faida za kuwepo kwa JKT. Basi
tuendelee kuliunga mkono Jeshi letu, lipate mafanikio makubwa zaidi miaka 50 ijayo.
Asanteni kwa kunisikiliza