Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kiwe ni kichocheo cha Vijana wa Kikristo kuwa
wafuasi wa Kristo na Wamissionari mahiri!
Nia ya jumla ya Baba Mtakatifu kwa Mwezi Julai inajikita zaidi katika Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 itakayoadhimishwa nchini Brazil, ili iwe
ni kichocheo kwa vijana wa Kikristo kuwa ni wafuasi wa Kristo na Wamissionari wa Injili.
Baba Mtakatifu
katika nia yake ya Kimissionari anaielekeza zaidi Barani Asia, ili liweze kufungua
malango yake kwa wajumbe wa Injili. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita,
katika Waraka wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Mlango wa Imani, “Porta
Fidei” anawaalika waamini kwa namna ya pekee, kuwa ni mng’ao wa Neno la Ukweli.
Hii ndiyo hija ya maisha iliyooneshwa na Kristo alipokutana na yule mwanamke
Msamaria pale kisimani, akamwomba maji ya uzima wa milele. Katika mahojiano na Yesu,
yule mwanamke akamfungulia Yesu hazina ya moyo wake naye Kristo akazima ile njaa na
kiu iliyokuwa imejikita katika moyo wa yule mwanamke, kiasi kwamba, akapata ari na
mwamko wa kwenda kuwashirikisha wengine ile furaha ya Habari Njema ya Wokovu inayobubujika
kwa kukutana na Yesu Kristo!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita,
anasema, hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya Wakristo kwa sasa, kwani wanahamasishwa
kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaozamisha mizizi katika maisha na
utume wa Kanisa. Waamini watambue kwamba, wao ndio walengwa wakuu wa Injili na pia
wanatumwa Kuwainjilisha wengine! Kiini cha Injili ni Yesu Kristo aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu na kwamba, Yeye ndiye Mkombozi wa dunia.
Yesu
ni Neno wa Mungu aliyetumwa ulimwenguni, akajitoa bila ya kujibakiza kwa njia ya Fumbo
la Umwilisho, kwa kujitwalia hali ya unyonge wa mwanadamu, akaupenda na kuukomboa
kutoka katika dhambi na mauti kwa njia ya Fumbo la Msalaba! Imani kwa Mwenyezi Mungu
ni kazi ya upendo iliyotekelezwa na Yesu na kwamba, hii ni zawadi na fumbo ambalo
linapaswa kukaribishwa moyoni na katika uhalisia wa maisha, kama alama ya shukrani
kwa Kristo.
Imani ni zawadi ambayo mwamini anaalikwa kuishirikisha kwa wengine;
ni karama inayopaswa kuendelezwa ili iweze kuzaa matunda; ni mwanga unaopaswa kung’ara
katika maisha ya watu! Hii ni zawadi muhimu sana katika historia na maisha ya mwanadamu
mintarafu uwepo wa Kristo anayeponya, safisha na kudhihirisha uwepo wake unaotuliza
shida na mahangaiko ya maisha ya mwanadamu.
Kutokana na changamoto zote hizi,
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anasema, waamini wanapaswa kuwa
makini zaidi na hali halisi kwa wakati huu, ili kuibua mbinu mkakati wa kichungaji
utakaoliwezesha Kanisa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa moyo na ari kubwa zaidi
kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kila
mwamini na Jumuiya ya Waamini inajikita katika Injili ya Kristo, hasa nyakati hizi
ambako kuna mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea sehemu mbali mbali za dunia.
Kati
ya changamoto kubwa zinazoukabili mchakato wa Uinjilishaji Mpya ni ukanimungu na watu
kumezwa mno na malimwengu. Lakini, hata katika mazingira na hali kama hii, anasema
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, cha ajabu ni kuona kwamba, kuna
watu wenye kiu na njaa ya uwepo wa Mungu, wanaosubiri kumegewa Mkate wa Uzima wa Milele
na Kupewa Maji yanayozima kiu ya maisha na utupu wa mwanadamu, kama ilivyokuwa kwa
yule mwanamke Msamaria.
Kwa ufupi hizi ndizo nia za jumla na za kimissionari
za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Julai.