2013-07-10 11:05:33

Caritas Afrika inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati


Makatibu wakuu wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Barani Afrika katika mkutano wao mkuu, uliohitimishwa hivi karibuni mjini Nairobi, wameonesha masikitiko yao makubwa kutokana na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na athari za machafuko ya kisiasa nchini humo.

Caritas Afrika kama sauti ya kinabii kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, inapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wa Afrika ya Kati kwa kuwataka wadau mbali mbali nchini humo, kuhakikisha kwamba, machafuko haya hayageuzwi kuwa ni vita ya kidini.

Caritas Afrika, inapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wote walioguswa kwa namna ya pekee na machafuko na vita inayoendelea Afrika ya Kati na wanaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha vita hii inayoendelea kuleta madhara makubwa kwa watu na mali yao.

Caritas Afrika inaliomba Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, Secam, katika mkutano wake wa kumi na sita, uliofunguliwa tarehe 9 na unatarajiwa kukamilika hapo tarehe 15 Julai 2013, kupitisha azimio la Makanisa Barani Afrika kuchangia kwa hali na mali wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Caritas katika mkutano wake, imeazimia kuhakikisha kwamba, inasambaza Waraka wa Kichungaji uliotolewa na Caritas Afrika katika mkutano wake uliofanyika Jimbo kuu la Kinshasa kunako mwaka 2012 kuhusu utambulisho wa Kimissionari katika mwanga wa Waraka wa Mungu ni upendo, ulioandikwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita sanjari na ule wa Asili ya Kanisa ni Huduma, uliotolewa pia na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.







All the contents on this site are copyrighted ©.